RAIS MAGUFULI AIBUKIA KWENYE GEREZA LA UKONGA DAR



RAIS John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, na kupiga marufuku uuzwaji wa sare za jeshi nchini kwa watu binafsi na kutaka wale wote wanaouza sare hizo wazikabidhi kwa jeshi husika mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Magufuli alifanya ziara hiyo ya kushtukiza jana jioni.

Ikulu imesema Rais Magufuli amepiga marufuku hiyo kutokana na maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kwamba wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi, kinyume cha taratibu za majeshi nchini.

Rais Magufuli amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za jeshi nchini.

“Hali kadhalika Rais Magufuli amepiga marufuku kwa majeshi yote nchini kuingia ubia na watu binafsi, kupangisha ama kuuza maeneo yao kwa ajili ya kufanya biashara na kutaka maeneo yote ya majeshi yabaki katika jeshi husika,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

“‘Haiwezekani sare za majeshi yetu hapa nchini kuuzwa na watu binafsi, hilo haliwezekani kamwe labda baada ya kumaliza muda wangu,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametoa Sh bilioni 10 kwa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujenga nyumba mpya zitakazotumika kwa ajili ya makazi ya askari wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Ikulu, inatokana na kilio cha askari Magereza kuwa wengi wao wamekuwa wakiishi uraiani, kitu ambacho ni tofauti na taratibu za majeshi nchini na hata kuzorotesha utendaji kazi wa askari wa jeshi hilo.

Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu pia ameagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha wafungwa wanatumika katika uzalishaji mali badala ya mfumo wa sasa ambao baadhi ya wafungwa wamekuwa wakitumia rasilimali za serikali bila kuzifanyia kazi.

Amewahakikishia maofisa na askari wa Jeshi la Magereza kuwa serikali itaendelea kuboresha maslahi yao na vitendea kazi kama inavyofanya kwa majeshi mengine nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527