JELA MWAKA 1 KWA KUMDHALILISHA KIMAUMBILE KWA MIKONO MAMA YAKE MZAZI

Mwanaume mkazi wa Ilala, Siwema Seif (40) amehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo ya Ilala kwenda jela mwaka mmoja kwa kumtolea lugha ya matusi na kumdhalilisha kimwili, Zainab Ramadhan ambaye ni mama yake mzazi.


Akisoma hukumu mahakamani hapo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Matrona Luanda alisema ushahidi uliotolewa na shahidi namba moja ambaye ni mlalamikaji, ulionesha kukosa shaka na kumtia hatiani mshitakiwa.


Shahidi huyo alisema siku ya tukio mshitakiwa alifika nyumbani kwao akaomba chakula akajibiwa kuwa kuna wali na mshitakiwa akasema hataki wali bali anataka ugali na mama akamjibu asingeweza kupika ugali na kumsisitiza Siwema ale wali.


Zainab alisema baada ya majibizano hayo, mshitakiwa alimtukana matusi ya nguoni mama yake, huku akisema hawezi kumzaa na kumkashifu, kwamba hana sehemu ya kumzalia huku akitishia kumwua akiahidi kumtoa roho ndipo amjue yeye ni nani.


Kwa mujibu wa Zainab, alipoona ugomvi na matusi umezidi aliingia chumbani mwake, na ndipo mlalamikaji akamfuata na kumtukana huku akitishia kumwingilia kinyume cha maumbile.


“Baada ya hapo mshitakiwa alinivamia na kunidhalilisha kimaumbile kwa mikono yake,” alisema.


Baada ya ushahidi wa mama huyo dhidi ya Siwema, Mahakama ilitoa nafasi kwa kijana huyo kujitetea na Mahakama ikamtia hatiani.


Karani wa mahakama hiyo, Blanka Shao alisema kwa kuwa mshitakiwa alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza na kitendo alichokifanya ni cha kifedhuli tena haonyeshi kujutia, alishauri apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwake.


Hakimu Luanda alimhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa kitendo alichomfanya mama yake mzazi.


Awali, ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 9 Ilala, mtaa wa Sophia Kawawa, nyumba namba 10.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527