JELA MIAKA 90 KWA KUTUMIA SILAHA YA KIVITA AK 47 KUPORA MILIONI 6..BADO KESI YA MAUAJI



MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imewahukumu watu watatu kutumikia kifungo cha miaka 90 jela baada kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupora zaidi ya shilingi milioni sita.

Washitakiwa hao ni Shaban Hamis (35) mkazi wa kijiji cha Ilunde wilayani Mlele , Masoud Ramadhani (33) mkazi wa kijiji cha Inyonga wilayani Mlele na Ramadhani Agustino (22) mkazi wa kijiji cha Kitunda mkoani Tabora ambapo kila mmoja atatumikia miaka 30 jela.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo , Teotimus Swai ametoa hukumu hiyo baada ya washitakiwa hao watatu kukiri makosa yao.

“Nimetoa adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho si kwao tu pia kwa wengine wenye tabia kama hiyo. Kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela kwa kila mshtakiwa,” amesema Hakimu Swai .

Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi , Baraka Hongoli amedai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Agosti 21,mwaka huu saa nane usiku katika Mtaa wa Uzenga mjini Inyonga ,wilayani Mlele .

Ilidaiwa kuwa usiku wa tukio washtakiwa hao wakiwa na silaha nzito aina ya AK 47 walivamia duka la mfanyabiashara , Jonas Davis katika Mtaa wa Uzenga na kumpora zaidi ya shilingi milioni sita.

Mwendesha Mashitaka huyo aliongeza kuwa washtakiwa hao walikamatwa Septemba 16 , mwaka huu wakiwa katika nyumba ya wageni, mtaa wa Isengo mjini Inyonga, wilayani Mlele wakijiandaa kuwapora fedha za wakulima wa tumbaku .

Ilidaiwa kuwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa walikiri kwa maandishi kuwa walihusika na uporaji wa shilingi milioni sita na wakawaongoza askari polisi hadi kijijini Ilunde na kuonesha walikoificha silaha aina ya AK 47.

Washitakiwa hao watatu pia walikabiliwa na mashitaka mengine ya kuvamia nyumba ya mkazi wa kijiji cha Kalonvya wilayani Mlele , Patrick Nchimbi na kumpora fedha taslimu, vitu vya thamani zikiwemo vocha za muda wa hewani , vitenge na simu za mkononi kwa pamoj vikiwa na thamani ya shilingi milioni 3.1 .

Washtakiwa hao watatu pia wanakabiliwa na kesi ya kumuua mfanyabiashara Jonas Davis kwa kumpiga risasi ambapo hawakutakiwa kujibu shtaka hilo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mauaji , ispokuwa Mahakama Kuu pekee.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527