
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara wenye lengo la kufuatilia, kukagua utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Novemba 8,2026 viwnaja vya SHIRECU
Na Sumai Salum-Kishapu
WAZIRI MKUU wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa wajawazito na wagonjwa wa dharura (ajali) wanapaswa kupatiwa huduma mara moja bila kucheleweshwa na taratibu za kiutawala, akionya kuwa uzembe huo unaweza kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.
Ameyasema hayo Novemba 8, 2026, katika mkutano wa hadhara wenye lengo la kufuatilia utekelzaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga uliofanyika Viwanja vya SHIRECU wilayani humo, huku akitoa mfano wa mama mjamzito anayefikishwa hospitalini akiwa na uchungu wa kujifungua lakini badala ya kuhudumiwa anaulizwa maswali yasiyo ya msingi kama “Beseni liko wapi?”, hali inayoweza kuchelewesha matibabu na kusababisha kifo, kisha kuhusishwa na mpango wa Mungu, akisema Serikali haitakubali mazoea hayo katika ofisi za umma.

Mhe. Mwigulu amezitaka hospitali kutowachangisha wagonjwa fedha za mafuta ya gari la wagonjwa wa dharura kwani ni huduma inayopaswa kutolewa na Serikali, akisisitiza kuwa kipaumbele ni kuokoa maisha.
"Na nyie baadhi yenu ambao mko kwenye maofisi ya Umma unakuta Mwananchi ametumia gharama kubwa na muda wake kutoka sehemu za mbali akija kupata huduma badala ahudumiwe haraka wewe unaendelea na kuchati na hata wakati mwingine kutohudumiwa kabisa madai hakuwa na miadi hatutawavumilia hata kidogo mtambue mko hapo kwa sababu ya wananchi" amesisistiza Mwigulu
Aidha amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Paschal Katambi, kuhakikisha wananchi wanaofanya makosa yanayostahili faini hawanyang'anywi wala kushikiliwa vyombo vyao vya moto, bali wanadaiwa faini na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao ili kuendelea kujiingizia kipato kiwasaidie wao na wanaowategemea.
"Utasikia Faini tu wamekimbizana askari na dereva matokeo yake kijana wa bodaboda ameanguka na kupoteza maisha, Dira ya Taifa inaeleza kuwa 70% ya mchango wa pato la taifa itatokana na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na hao bodaboda, Mamalishe na wengine hivyo msishikirie vyombo vyao ni kuwapotezea muda na kutesa familia zao na wanaowategemea mkatie faini muache aendelee na kazi ili ailipe" Amesema
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameitaka Wizara ya Ujenzi kuharakisha uhuishaji wa usanifu wa barabara ya Kolandoto–Mwangongo ili iingizwe katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028, huku maandalizi yakizingatia madaraja, njia itakayopita na fidia kwa wananchi watakaoguswa.
"Ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi hii hapo awali ilikuwa ni kutokana na fedha zikitoka zinapitia Wizara ya fedha lakini sasa serikali imeamua fedha zote za miradi ya maendeleo itaenda moja kwa moja kwenye mifuko ya maendeleo na hapo itasaidia kuharakisha ujenzi wa barabara zetu ili kuondoa changamoto hii" Amesisistiza
Awali, Mbunge wa Kishapu, Lucy Thomas Mayenga, amesema usanifu wa barabara hiyo ulifanyika mwaka 2017, lakini wananchi wameendelea kukabiliwa na changamoto za usafiri, uharibifu wa bidhaa na kuchelewa kuwafikisha wagonjwa hospitalini.
Kuhusu kilimo cha pamba, ametangaza kuwa msimu ujao utakuwa na wanunuzi mbalimbali badala ya mnunuzi mmoja ili kuongeza ushindani na kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri, akizingatia malalamiko yaliyowasilishwa na wakulima na madiwani kupitia Mbunge Mayenga.
Vilevile, ameitaka Wizara ya Maji kuzingatia maeneo yenye ukame katika kupanga miradi, ikiwemo Kishapu, huku akiahidi kuitisha taarifa kuhusu suala la ufufuaji wa kiwanda cha SHIRECU.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Patrobas Katambi
Waziri wa ujenzi Mhe. Masanja Kadogosa
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Wycliffe Makamba
Mbunge wa Jimbo la kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga
Katibu Tawala Mkoani Shinyanga Pili Mnyema
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi(Katikati), Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro(wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Dkt. Francis Mlacha(wa kwanza Kulia)
Katibu Tawala Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Niceforus Mgaya(aliyevalia koti na shati nyeupe)



TAFUTA HABARI
Social Plugin