
Na: OWM–TAMISEMI, Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka Wakuu wa Mikoa kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao ya utawala kwa kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma bora, usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo Novemba 29, 2026, wakati wa kikao kazi na Wakuu wa Mikoa katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma, ambapo amewataka viongozi hao kurejea katika maeneo yao ya utawala na kuhakikisha wanawapa kipaumbele wananchi kwa kuwasikiliza na kutatua kero zao, ili kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kupeleka tabasamu la kudumu kwa wananchi.
Prof. Shemdoe amewasisitiza viongozi hao kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya utawala, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Sanjali na hilo, Prof. Shemdoe amewasisitiza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kwenda kutekeleza kwa uharaka na ufanisi maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Novemba 27, 2026 wakati alipokuwa akiwaapisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na viongozi aliowateuwa Novemba 25, 2026.
Aidha, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumtambulisha kwa Wakuu wa Mikoa Katibu Mkuu wa OWM–TAMISEMI, Bw. Eliakimu Maswi, ambaye ameahidi kushirikiana na viongozi hao katika kuhakikisha Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinatekeleza majukumu yake kikamilifu.
Katika kuhakikisha maelekezo ya Mhe. Rais yanatekelezwa, Prof. Shemdoe alimuhimiza Katibu Mkuu Maswi kukaa na Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweka mikakati madhubuti ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, na ya uchukuaji wa hatua dhidi ya watakaobainika kutotekeleza majukumu yao na maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais.
Kikao kazi hicho kimefanyika mara baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kufanya kikao kazi na Mawaziri wa Kisekta pamoja na Wakuu wa Mikoa katika ukumbi huo wa Hazina, kilicholenga kuimarisha uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya kisekta, yakiwemo masuala ya ulinzi na usalama katika mikoa yote nchini.











TAFUTA HABARI
Social Plugin