
Makamu wa Rais , Deogratias Ndejembi akifungua kwa niaba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa saba wa Kimataifa wa Uwekezaji kwenye sekta ya Madini Tanzania (TIMC) uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni

Makamu wa Rais , Deogratias Ndejembi akipokea tuzo baada ya ufunguzi wa Mkutano wa saba wa kimataifa wa Uwekezaji kwenye sekta ya madini Tanzania kutoka kwa Waziri wa Madini , Anthony Mavunde jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu , Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia) akimpa tuzo Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt Melkiory Ngido ya kutambua mchango wa Barrick kwenye Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) , utunzaji wa mazingira na kwenye kuchangia maendeleo ya nchini , kati kati ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde
Na Damas Makangale, Dar es Salaam
Siku za hivi karibuni, utajiri mkubwa wa madini wa Tanzania umekuwa ukitajwa kama moja ya nguzo muhimu za uchumi wa taifa, ukichangia mapato ya Serikali, fedha za kigeni, ajira na uwekezaji.
Hata hivyo, katika kipindi hiki kipya cha maendeleo, Serikali inalenga kwenda hatua nyingine kubwa zaidi—kuhakikisha utajiri huo hauishii kwenye uchimbaji na usafirishaji wa madini, bali unatumika kujenga viwanda, kuongeza ajira, kuhamisha teknolojia na kuleta manufaa mapana kwa watanzania wote.
Hii ndiyo agenda iliyotawala Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (TIMC 2026), uliowakutanisha washiriki takribani 1,715, wakiwemo 226 kutoka nje ya Tanzania na zaidi ya wazungumzaji 57.
Mkutano huo uliweka wazi dhamira ya Tanzania ya kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi ili kukuza mnyororo wa thamani na kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali hizo.
Kwa mtazamo mpana, ujumbe wa mkutano ulikuwa mmoja: Tanzania haitaki tena kutambulika pekee kama nchi inayochimba dhahabu, tanzanite, nickel, graphite, kobalti na madini mengine, bali inataka kuwa nchi inayoongeza thamani ya madini hayo na kuzalisha bidhaa zinazotokana nayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi mwelekeo huo akisema lengo ni kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na rasilimali za madini kupitia uongezaji thamani wa madini nchini.
“Lengo langu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wengi zaidi wananufaika na rasilimali zetu za madini kupitia uongezaji thamani wa madini nchini kwa ukamilifu,” alisema Rais Samia, akibainisha kuwa Tanzania tayari imeanzisha viwanda vya kusafisha madini ambavyo vimewezesha kufikia kiwango cha usafi wa asilimia 99.99 kwa dhahabu na fedha.
Rais Samia pia amesisitiza kuwa ajenda ya taifa ya maendeleo ya viwanda haiishii kwenye dhahabu, bali inahusisha madini ya kimkakati na muhimu kama shaba, kobalti, nikeli na chuma, ambayo Tanzania imejaaliwa kwa wingi.
Kutoka uchimbaji kwenda uongezaji thamani.
Hapa ndipo kunapoonekana mabadiliko makubwa katika mtazamo wa Serikali kuhusu sekta ya madini.
Kwa miaka mingi, changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika imekuwa kuchimba malighafi na kuziuza nje, kisha kununua bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo kwa bei kubwa zaidi.
Tanzania sasa inataka kuvunja mzunguko huo kwa kuwekeza katika uchechuaji, uyeyushaji, usafishaji, uchakataji na hatimaye utengenezaji wa bidhaa za madini.
Tayari Serikali imeelekeza eneo la Mgodi wa Barrick - Buzwagi ambao uko katika hatua za mwisho za kufungwa, kuwa eneo linaloweza kutumika kwa shughuli za kuongeza thamani na uzalishaji wa bidhaa zinazohusiana na madini.
Aidha, Tanzania ina viwanda vinane vya kusafisha dhahabu, huku viwanda vingine zaidi ya 16 vya uchakataji, hususan wa shaba na nikeli, vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Hii inaashiria mabadiliko kutoka mfumo wa “kuchimba na kuuza” kwenda kwenye mnyororo mpana unaoweza kuonekana kama: madini, uchimbaji, uchakataji, usafishaji, utengenezaji na bidhaa ya mwisho.
Kadiri Tanzania inavyosogea kuelekea mwisho wa mnyororo huo, ndivyo uwezekano wa fedha nyingi zaidi, ajira, teknolojia na ujuzi kubaki nchini unavyoongezeka kwa kasi.
Madini kama injini ya viwanda
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratias Ndejembi, amesema sekta ya madini haiwezi kuendelea kuwa sekta inayojitegemea bila kuhusishwa na sekta nyingine za uchumi.
Amesema ni muhimu wadau kuhakikisha sekta hiyo inafunganishwa na sekta nyingine mtambuka ili kuchochea ukuaji wa uchumi na mnyororo wa thamani.
Kwa mujibu wa Ndejembi, madini yanaweza kuchochea ukuaji wa kilimo, viwanda na nishati, huku uongezaji thamani ukisaidia kuongeza mapato ya Serikali, ajira na fursa za kiuchumi kwa watanzania wengi zaidi.
Hivyo, mnyororo unaotarajiwa si wa madini pekee. Ni mfumo mpana unaoweza kuunganisha madini na viwanda, nishati, usafirishaji, ujenzi, benki, bima, teknolojia ya habari na mawasiliano, elimu, utafiti, kilimo na biashara.
Kwa maana hiyo, sekta ya madini inaweza kuwa injini ya ukuaji wa viwanda badala ya kuwa chanzo cha mapato ya serikali pekee.
Critical minerals na fursa mpya
Mkutano huo pia uliweka uzito kwenye madini muhimu na ya kimkakati, ambayo mahitaji yake yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya teknolojia na uchumi wa dunia.
Madini kama nickel, cobalt, graphite, copper na mengine yanazidi kuwa muhimu katika uzalishaji wa magari ya umeme, betri, nishati jadidifu, vifaa vya kielektroniki na viwanda vya kisasa.
Kwa Tanzania, hii ni fursa ya kimkakati.
Nchi inaweza kutumia utajiri wake wa madini kuvutia wawekezaji katika uchimbaji, uchakataji, teknolojia, uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na madini hayo.
Lakini fursa hiyo haiwezi kutimia kwa kuwa na madini pekee. Inahitaji mtaji, teknolojia, wataalamu, miundombinu, nishati ya uhakika na masoko.
Ndiyo maana mjadala wa TIMC 2026 ulihusisha kwa kiasi kikubwa masuala ya uwekezaji, teknolojia, miundombinu, rasilimali watu na ushindani wa kimataifa.
Watanzania lazima wawe sehemu ya mnyororo
Mabadiliko hayo hayawezi kuwa na maana kubwa iwapo yatabaki kwenye kiwango cha viwanda na wawekezaji bila kuwafikia wananchi.
Hii ndiyo sababu Serikali imekuwa ikisisitiza ushiriki wa watanzania kupitia sera na kanuni ya Maudhui ya Ndani (Local Content), huku wanawake, vijana na makundi mengine wakitakiwa kutumia fursa zinazotokana na sekta hiyo.
Ndejembi amesema sekta ya madini inapaswa kufungua milango kwa vijana na wanawake kushiriki katika ajira na zabuni zinazotolewa na migodi, kupitia utekelezaji wa sera na kanuni za Maudhui ya Ndani.
Kwa upande mwingine, wachimbaji wadogo nao wamepewa nafasi katika mjadala wa mnyororo wa thamani.
Lengo ni kuwawezesha kutoka katika uchimbaji wa kiwango cha chini unaokabiliwa na changamoto za teknolojia, mitaji na masoko na kuwa sehemu ya mfumo mpana wa uchakataji na biashara ya madini.
Mafanikio yapimwe kwa maisha ya wananchi.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameweka kipimo kingine muhimu cha mafanikio ya sekta hiyo.
Amesema historia haitawakumbuka Watanzania kwa kiasi cha madini waliyochimba kutoka ardhini, bali kwa namna walivyotumia utajiri huo kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
Kauli hiyo inabadilisha mjadala kutoka kwenye takwimu za uzalishaji na mapato ya kodi pekee kwenda kwenye maswali muhimu zaidi: ni ajira ngapi zimezalishwa? Ni viwanda vingapi vimejengwa? Ni teknolojia kiasi gani imehamishwa? Ni biashara ngapi za Watanzania zimekua? Na ni kwa kiwango gani wananchi wanaona manufaa ya rasilimali zilizopo nchini?
Kwa takwimu zilizotolewa kwenye mkutano, sekta ya madini inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa na imeingiza takribani dola bilioni 5.40 za Marekani katika fedha za kigeni.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tanzania inaendelea kuwa kinara katika kuchangia uchumi na uanzishwaji wa viwanda vya uchakataji na usafishaji madini.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema mapato kutoka sekta hiyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 506 mwaka 2023/24 hadi Sh trilioni 1.39 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Hata hivyo, hatua inayofuata ni kuhakikisha ongezeko hilo la mapato linaenda sambamba na ongezeko la thamani ya madini, viwanda, ujuzi, ajira na biashara za ndani.
Nafasi ya Barrick-Twiga
Katika utekelezaji wa ajenda hiyo, wawekezaji wakubwa kama Barrick kupitia ubia wake na Serikali wa Twiga Minerals wanaendelea kuwa sehemu ya sekta hiyo.
Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema tangu kuanza kwa usimamizi wa migodi ya Barrick nchini mwaka 2019, kampuni hiyo imeingiza zaidi ya Sh trilioni 16 katika mzunguko wa uchumi wa ndani.
Kwa mwaka 2025 pekee, alisema mchango wa kampuni hiyo ulifikia takribani Sh trilioni 2.2, huku Sh trilioni 4.7 zikilipwa kama kodi na zaidi ya Sh bilioni 700 zikilipwa kwa Msajili wa Hazina kama gawio la Serikali.
Aidha, migodi ya Barrick-Twiga ya North Mara na Bulyanhulu ina zaidi ya wafanyakazi 6,400, ambapo asilimia 95 ni Watanzania na asilimia 77.7 wanatoka maeneo yanayozunguka migodi hiyo.
Kampuni hiyo pia imeendelea kuwekeza katika miundombinu na huduma za jamii, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kahama-Kakola yenye urefu wa kilomita 73 na programu ya elimu ya Barrick-Twiga Forward Future Education inayolenga kuboresha miundombinu ya shule za sekondari.
Changamoto iko kwenye utekelezaji
Pamoja na dhamira hiyo, swali kubwa sasa si kama Tanzania ina utajiri wa madini. Swali ni kama inaweza kubadilisha utajiri huo kuwa uwekezaji halisi, viwanda, ajira na biashara endelevu.
Ili hilo litokee, nchi inahitaji sera na sheria zinazotabirika, miundombinu imara, umeme wa uhakika, mitaji, teknolojia, wataalamu, masoko na mazingira rafiki ya biashara.
Taarifa ya Wizara ya Madini ikinukuu Fraser Institute inaonyesha Tanzania ilishika nafasi ya nne barani Afrika katika Investment Attractiveness Index ya mwaka 2025, huku alama yake ikipanda kutoka 46.38 mwaka 2023 hadi 68.04 mwaka 2025.
Hii ni hatua muhimu, lakini kipimo kikubwa zaidi sasa kitakuwa namna mvuto huo unavyobadilishwa kuwa viwanda vinavyofanya kazi, ajira, teknolojia na biashara zinazowanufaisha Watanzania.
Afrika nayo inatafuta mabadiliko
Kwa kiwango cha bara, agenda ya Tanzania inaendana na matarajio mapana ya Afrika ya kubadilisha utajiri wa madini kuwa utajiri wa viwanda.
Badala ya mfumo wa Afrika kuchimba, kusafirisha malighafi na baadaye kuagiza bidhaa zilizotengenezwa nje, matarajio ni kujenga mfumo ambao Afrika inachimba, inachakata, inazalisha na hatimaye kuuza bidhaa zenye thamani kubwa zaidi.
Hii inaweza kuongeza uwezo wa nchi za Afrika kujadiliana katika soko la dunia, kuongeza biashara ndani ya bara na kupunguza utegemezi wa kuuza malighafi.
Kwa hiyo, TIMC 2026 haikuwa tu mkutano wa kutafuta wawekezaji wa migodi. Ujumbe wake mpana ulikuwa kwamba Tanzania na Afrika zinataka sehemu kubwa zaidi ya thamani inayotokana na madini ibaki ndani ya bara.
Ndoto inayosubiri utekelezaji
Mwisho wa yote, ndoto ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya madini inaweza kutimia iwapo kauli kuhusu uongezaji thamani, viwanda, ajira na mnyororo wa thamani zitageuzwa kuwa miradi halisi.
Tanzania tayari ina rasilimali, wawekezaji, uzoefu wa uchimbaji na msingi unaokua wa viwanda vya uchakataji na usafishaji. Kinachohitajika sasa ni kuongeza kasi ya hatua inayofuata.
Kama madini yataunganishwa kwa ufanisi na viwanda, nishati, usafirishaji, fedha, teknolojia, elimu, utafiti na biashara, sekta hiyo inaweza kuwa moja ya injini kuu za Tanzania ya viwanda.
(Industrialization drive)
Hapo ndipo mafanikio ya kweli yatakapopimwa—si kwa tani za madini zinazochimbwa pekee, wala kwa mapato yanayoingia Serikalini pekee, bali kwa idadi ya viwanda vinavyojengwa, ajira zinazozalishwa, teknolojia inayobaki nchini, biashara zinazokua na maisha ya watanzania yanayobadilika siku hadi siku.
Kwa kifupi, Tanzania sasa inalenga kubadilisha utajiri wa madini kuwa utajiri wa viwanda.
Na kama ndoto hiyo itatekelezwa kwa vitendo, madini yanaweza kuwa zaidi ya rasilimali ya chini ya ardhi—yanaweza kuwa msingi wa uchumi mpana, wenye ajira, teknolojia, viwanda na fursa kwa kizazi kijacho.
TAFUTA HABARI
Social Plugin