Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OUT YAIMARISHA UWEZO WA TAASISI ZA UMMA KATIKA UFUATILIAJI NA TATHMINI


Na Mwandishi Wetu- Morogoro

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kupitia Ofisi yake ya Ushauri wa Kitaalamu (OCB), kinaendesha mafunzo ya uandaaji wa Mpango wa Mwaka wa Ufuatiliaji na Tathmini na Mwongozo Tendaji wa Ufuatiliaji na Tathmini mjini Morogoro.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu ya pili yalianza tarehe 10 Novemba 2026 na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Novemba 2026, yameshirikisha washiriki kutoka mamlaka za serikali za mitaa na sekretariati za mikoa ya Simiyu, Iringa na Pwani.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa chuo Kikuu huria (OUT) Prof. Alex Makulilo amesema, mafunzo hayo yamejikita katika kazi za vitendo, ambapo washiriki wanaandaa nyaraka za taasisi kwa msaada wa wawezeshaji wa Chuo Kikuu Huria (OUT).

Aidha, amesema, washiriki wanajifunza kuandaa viashiria vya kupima utendaji, zana za kukusanya taarifa na utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo.

"Kila taasisi inayoshiriki inatarajiwa kuondoka na rasimu ya Mpango wa Mwaka wa Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Mwongozo Tendaji kwa ajili ya kukamilishwa na kutumika" amesema Prof. Alex Makulilo.

Ameendelea kusema kwamba, Mwongozo huo utaweka taratibu za kukusanya na kuchambua taarifa, kutoa taarifa za utekelezaji na kutumia matokeo katika maamuzi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Tanzania Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Sakina Mwinyimkuu, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Bi. Ashura Selemani, amesema matumizi ya nyaraka hizo zitaboresha ufuatiliaji na tathmini kwa kuweka utaratibu unaoeleweka wa kupima utekelezaji na kubaini mapungufu mapema.

Nae Mratibu wa mafunzo hayo, Dk. Emmanuel Mallya, ameeleza kuwa awamu ya tatu ya mafunzo hayo itafanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 4 Desemba 2026, ambapo awamu hiyo itahusisha mamlaka za serikali za mitaa na sekretariati za mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Mara, Kilimanjaro, Arusha na Katavi. Pia itazihusisha halmashauri nyingine ambazo, kwa sababu mbalimbali, hazikuweza kuhudhuria awamu zilizopita.

Hata hivyo Mwisho wa mafunzo hayo, Chuo kitaandaa taarifa rasmi itakayowasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com