
Na Mwandishi wetu,Arusha.
Wakulima na wadau wa sekta ya kilimo nchini wametakiwa kutumia maonesho ya kimataifa ya Hortilogistica kama jukwaa la kujifunza teknolojia mpya, kuongeza thamani ya mazao na kujenga mahusiano ya kibiashara yatakayowawezesha kufikia masoko ya kimataifa.
Maonesho hayo yameanza leo Novemba 8, 2026, katika viwanja vya TGT Club jijini Arusha na yanatarajiwa kuhitimishwa Novemba 10, 2026. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maonesho hayo yanayofanyika jijini Arusha kwa mara ya kwanza.
Akizungumza leo novemba 08,2026 Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amewakaribisha wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki maonesho hayo, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa wakulima, wazalishaji na wawekezaji kukutana, kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano utakaosaidia kukuza sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya maonesho hayo, Mhe. Chongolo amesema Hortilogistica ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha wadau wa kilimo na kuwafungulia wakulima fursa za kupata masoko ya mazao ya bustani katika ushindani wa kimataifa.
Amesisitiza umuhimu wa wakulima kuongeza uzalishaji na kuzingatia ubora wa mazao ili waweze kunufaika na fursa za masoko ya kimataifa, akitaja zao la parachichi kuwa miongoni mwa mazao yenye fursa kubwa katika biashara hiyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wadau wa kilimo walioshiriki maonesho hayo, wakiwemo kutoka kampuni ya Africado, wamesema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuonesha teknolojia, bidhaa na huduma mbalimbali za kilimo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo.
Wamesema mwitikio wa wadau katika maonesho hayo ni mkubwa, huku wakieleza kuwa wanatarajia kuyatumia maonesho hayo kuwafikia wakulima wengi zaidi ndani na nje ya nchi kupitia kubadilishana uzoefu na teknolojia za uzalishaji.
Aidha, wameeleza kuwa uwezo wa uzalishaji wa miche umeongezeka kutoka miche 10,000 hadi kufikia miche 200,000 kwa mwaka, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa miche na kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani nchini.










TAFUTA HABARI
Social Plugin