Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UELEWA MDOGO WA HUDUMA ZA UTAMBUZI WA WATOTO WAWANYIMA MATUMAINI WAZAZI GEITA


Wazazi wa Mtaa wa Molinge wakiwa na Afisa Mtendaji wa mtaa huo mara baada ya kumaliza kuongea na mwandishi wa habari
 ***

#Wazazi na wadau wa watoto wenye mahitaji maalum wanakosa taarifa za kutosha kuhusu huduma za upimaji wa awali, huku hospitali zikiendelea kuwa tegemeo lao.

Na Theresia Method, Geita

“Tuna ndoto za kuwa madaktari, tuna ndoto za kuwa mapiloti, tuna ndoto nyingi za maisha, tuwezeshwe tunaweza.”

Maneno hayo kutoka katika wimbo wa msanii Kala Jeremiah yanabeba matumaini ya watoto wanaotamani kutimiza ndoto zao. Hata hivyo, kwa baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum, safari ya kufikia ndoto hizo inaweza kukumbwa na vikwazo vinavyoweza kupunguzwa kwa kupata utambuzi wa mapema, huduma zinazofaa na mazingira rafiki ya kujifunzia.

Miongoni mwa wanaotamani kuona watoto wanapata fursa hizo ni Yohana Saiboke, mkazi wa Mtaa wa Molinge Mkoani Geita, ambaye ana ulemavu wa miguu na hutumia kiti mwendo.

Yohana anakumbuka namna alivyokosa fursa ya kupata elimu alipokuwa akikua kutokana na unyanyapaa, miundombinu isiyofikika kwa urahisi na mila potofu. Sasa, akiwa baba wa mtoto mmoja, ana matumaini kwamba mwanawe hatapitia changamoto kama alizokutana nazo yeye.

Mtoto wake anatarajiwa kuanza elimu ya awali mwaka 2027. Hali hiyo imemfanya Yohana kutamani mwanawe aanze shule katika mazingira yatakayomwezesha kujifunza na kukua bila vikwazo vinavyoweza kuzuilika.

Hata hivyo, anasema hajawahi kusikia kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto.“Sijawahi kusikia kuhusu vituo hivyo. Ila watoto wanapohitaji kupimwa, tunawapeleka hospitalini,” anasema Yohana.

Kwa Yohana, kupata taarifa sahihi kuhusu huduma hizo ni hatua muhimu ya kuhakikisha mwanawe anapata msaada unaohitajika kabla ya kuanza shule, endapo uchunguzi utaonesha kuwa anauhitaji.

Watoto wenye ulemavu

Changamoto ya kutofahamu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto haimhusu Yohana pekee. Marco Rozalia, ambaye pia hutumia kiti mwendo, anasema hajawahi kusikia kuhusu vituo hivyo na hakupata nafasi ya kwenda shule alipokuwa mtoto.“Sijawahi kusikia kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto. “Katika maisha yangu ya utotoni, sijawahi kwenda shule,” anasema Marco.

Kwa mujibu wa Marco, mazingira ya vijijini yanaweza kuwa kikwazo kwa watoto wenye mahitaji maalum kupata fursa sawa za elimu, hasa pale huduma na miundombinu isipokidhi mahitaji yao.

Anasema huduma za utambuzi na upimaji wa awali zikisogezwa karibu na jamii zinaweza kuwasaidia watoto kupata msaada unaofaa na kuongeza nafasi zao za kufikia malengo yao.“Vingesaidia sana. Watoto wengi wangesoma na kupata elimu nzuri, jambo ambalo lingewasaidia kutimiza malengo yao,” anasema Marco.

Ushuhuda wa Yohana na Marco unaonesha umuhimu wa kutoa taarifa kwa jamii kuhusu huduma zinazolenga watoto wenye mahitaji maalum. Hata hivyo, uelewa wa wananchi ni sehemu moja tu ya suala hili; upatikanaji wa huduma, urahisi wa kuzifikia na uwezo wa vituo kutekeleza majukumu yake pia ni mambo yanayohitaji kuangaliwa.

Wadau wa watoto waibua changamoto

Sofia Njete, Afisa Mradi wa Mtoto Kwanza mkoani Geita kutoka shirika la NELICO, anasema katika shughuli zao wamekuwa wakitumia hospitali za wilaya kupata huduma kwa watoto. Hata hivyo, hajawahi kutembelea kituo cha utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto mkoani humo.Anasema anatamani huduma hizo zipatikane katika mazingira rafiki na yanayoweza kufikiwa kwa urahisi na watoto pamoja na wazazi wao.

Sofia Njete Afisa Mradi wa Mradi wa Mtoto Kwanza Mkoa wa Geita kutoka shirika la NELICO.

“Tunaambiwa vituo vinapatikana pia katika hospitali za rufaa. Tulikuwa tunatamani huduma hizi ziwe mashuleni, lakini kwa sasa tunaamini kituo kipo katika hospitali yetu ya rufaa, ingawa sijabahatika kukitembelea,” anasema Sofia.

Sofia anasema wakati mwingine mtoto anaweza kuchukuliwa kuwa hafanyi vizuri darasani au haelewi masomo, ilhali tatizo linalomkabili linahitaji kutambuliwa na kushughulikiwa kwa msaada wa wataalamu.

“Ni changamoto kubwa kwa sababu mtoto anaweza kuwa na tatizo tangu kuzaliwa, lakini mzazi akashindwa kulitambua mapema. Wazazi wengi wanakuja ofisini kwetu kuuliza kwa nini mtoto wao hasomi kama wengine. Baadaye tunagundua kuwa mtoto hasikii vizuri au haoni vizuri, wakati mwingine baada ya kuwa ameadhibiwa mara nyingi,” anasema Sofia.

Kauli hiyo inaonesha umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata tathmini inayofaa, badala ya kuhukumiwa kwa namna wanavyojifunza au kushiriki darasani kabla ya kuelewa mahitaji yao.

Kwa upande wake, Methew Daniel, Mkurugenzi wa Bright Light Organisation, lililopo eneo la Mseto Mkoani Geita, anasema ameshiriki semina kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto na kufuatilia huduma hizo katika mikoa mingine, ikiwemo Dar es Salaam. Hata hivyo, anasema hajafuatilia wala kukiona kituo kinachotoa huduma hizo Geita.

“Nimeshiriki semina kadhaa kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto kwa sababu katika masuala ya watoto nataka kujifunza mengi zaidi ili niweze kutoa huduma pana zaidi. Kwa upande wa Geita, sijafuatilia, lakini katika mikoa mingine kama Dar es Salaam nimeweza kufuatilia,” anasema Methew.

Dkt. Methew Daniel, Mkurugenzi wa shirika la Bright LightOrganisation 

Shirika lake linahudumia watoto wenye mahitaji maalum, wakiwemo watoto wenye ualbino wanaokabiliwa na changamoto za uoni hafifu, pamoja na watoto wenye ulemavu wa viungo na usikivu.

Methew anasema amekuwa akitegemea hospitali kupata huduma za uchunguzi kwa watoto anaowalea. Kutokana na kutofahamu mahali kituo cha utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto kilipo Geita, anahoji namna huduma hizo zinavyowafikia wananchi wanaopaswa kunufaika nazo.

“Kwa upande wa Geita, sijawahi kukiona. Wenye vituo wanapaswa kujitafakari na kujiuliza kama vituo walivyoanzisha vinawanufaisha wao wenyewe au jamii,” anasema.

Hata hivyo, kutokufahamu kwa baadhi ya wadau mahali kituo kilipo hakuthibitishi moja kwa moja kuwa kituo hicho hakipo au hakifanyi kazi. Kinachoonekana ni haja ya kutoa taarifa zilizo wazi kuhusu mahali huduma zinapotolewa, utaratibu wa kuzipata na huduma zinazopatikana.

Takwimu za Elimu Geita

Kwa mujibu wa takwimu za elimu za mwaka 2024, zinazojulikana kama Basic Education Statistics in Tanzania (BEST 2024), wanafunzi 354 wenye ulemavu walikuwa wakisoma katika shule za serikali na zisizo za serikali mkoani Geita. Kati yao, wavulana walikuwa 208 na wasichana 146.Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanafunzi 115 walikuwa na ulemavu wa viungo vya mwili, wanafunzi 95 walikuwa na ulemavu wa akili, 30 walikuwa na uoni hafifu na 26 walikuwa na ualbino.

Aidha, wanafunzi 24 walikuwa na usikivu hafifu, 20 walikuwa na uziwi na 23 walikuwa na ulemavu wa aina nyingi. Wanafunzi 14 walikuwa na upofu, sita walikuwa na usonji, huku mwanafunzi mmoja wa kike akiwa na uziwi na upofu kwa pamoja.Takwimu hizi zinaonesha idadi ya wanafunzi wenye ulemavu waliorekodiwa katika shule mwaka 2024. Hata hivyo, hazibainishi idadi ya watoto wote wenye ulemavu mkoani Geita wala idadi ya watoto wanaohitaji huduma za vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto.

Jamii yataka huduma zisogezwe karibu na watoto

Kwa upande wa viongozi wa jamii, uelewa mdogo kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto unaweza kuchangiwa na mazoea ya wananchi kutegemea hospitali wanapohitaji huduma za afya na uchunguzi wa watoto.Meshaki Katambi, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Molinge, anasema anaamini wananchi wengi hawana taarifa za kutosha kuhusu vituo hivyo.

Meshaki Katambi, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Molinge

“Sidhani kama wananchi wanaelewa kuhusu vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto kwa sababu wamezoea kwenda hospitalini moja kwa moja. Kituo kikiletwa hapa, wataalamu wanaweza kuelimisha jamii na kuwasaidia wananchi kufahamu huduma hizo,” anasema Meshaki.

Anasema ofisi yake ina takwimu za zaidi ya watoto saba wenye mahitaji maalum katika Mtaa wa Molinge. Anasisitiza pia umuhimu wa jamii kutowaficha watoto wenye ulemavu ndani ya nyumba, bali kuwasaidia kupata elimu na huduma zinazohitajika.“Vituo hivi vikijengwa katika kila mtaa, vitasaidia watoto wenye ulemavu waliopo katika maeneo yetu kufika shuleni na kupata huduma bila usumbufu mkubwa,” anasema.

Ingawa ombi la kujenga vituo katika kila mtaa linaonesha matarajio ya jamii ya kupata huduma zilizo karibu, bado kuna umuhimu wa kuelewa mfumo rasmi wa utoaji wa huduma hizo na namna watoto wanavyoweza kufikishwa kwa wataalamu.Itwene Lyaki, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Geita, anasema watoto wanaohitaji uchunguzi wanaweza kupelekwa katika hospitali au vituo vya afya vilivyo karibu na maeneo wanayoishi, kisha kupelekwa hospitali ya wilaya kwa vipimo zaidi.

“Tunatumia hospitali yetu ya wilaya na vituo vya afya katika maeneo ya jirani. Watoto wanapobainika kuwa wanahitaji uchunguzi, huletwa hospitali ya wilaya kwa ajili ya vipimo zaidi,” anasema Lyaki.

Mwongozo wa Serikali

Mwongozo wa Serikali wa mwaka 2022 uliotajwa katika taarifa hii, vituo vya utambuzi, upimaji na rasilimali za elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinavyolenga utambuzi na upimaji wa awali wa watoto vilianzishwa kwa lengo la kusogeza huduma za utambuzi na upimaji wa awali karibu na jamii. Lengo ni kusaidia watoto kutambuliwa mapema na kupatiwa huduma zinazostahili bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda ngazi za mikoa au taifa kutafuta huduma hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com