Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SGR KUPUNGUZA MSONGAMANO BANDARINI, BARABARANI PROFESA MBARAWA




Na Sheila Ahmadi, Dodoma

Serikali Kupitia wizara ya uchukuzi imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Tanzania (TASAC) kushirikiana kuboresha huduma za usafirishaji wa mizigo kupitia reli ili kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na barabara za jiji hilo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha kusafirishia Makasha ya mizigo kwenye reli ya kisasa SGR kutoka Bahi mkoani dodoma Waziri Wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema matumizi ya kituo cha Bahi yameongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo wakati ujenzi wa vipande vingine vya reli ya SGR ukiendelea.

kwa sasa treni za mizigo kutoka Mkoani Dar es Salaam zinatumia takribani saa tano kufika Bahi ambapo mizigo inahamishiwa kwenye treni za MGR kwa ajili ya kuendelea na safari kuelekea maeneo ambayo reli ya SGR bado haijafika.

Aidha matumizi ya reli katika kusafirisha mizigo ni muhimu katika kupunguza utegemezi wa malori yanayotumia barabara kutoka bandarini kwenda maeneo mbalimbali nchini.

" Bandari ya Dar es Salaam hushughulikia zaidi ya kontena 3,000 kwa siku, hali inayohitaji kuimarishwa kwa njia mbadala za usafirishaji ili kukabiliana na ongezeko la mizigo "Amesema Profesa Mbarawa.

Katika hatua nyingine Peofesa mbarawa amezitaka taasisi husika kushirikiana na wadau wa sekta ya usafirishaji katika kuweka utaratibu utakaowawezesha wateja kukamilisha taratibu za nyaraka na malipo ya usafirishaji wa mizigo hadi vituo vya ndani badala ya kutegemea huduma hizo kufanyika bandarini pekee.

Vilevile hatua hiyo itasaidia kupunguza safari za malori kwenda na kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa shughuli za biashara.

Nitoe Wito kwa TPA, TRC na TASAC kujifunza uzoefu kutoka nchi nyingine, ikiwamo Misri, ambako kuna mifumo ya vituo vya ndani vinavyotumika kupokea na kusambaza mizigo kutoka bandarini.

Pia ameipongeza TRC kwa ubunifu wa kuanzisha utaratibu wa kuhamisha mizigo kati ya reli ya SGR na MGR katika Kituo cha Bahi, akisema hatua hiyo imewezesha mizigo kuendelea na safari bila kusubiri kukamilika kwa ujenzi wa reli ya SGR hadi Isaka.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli Tanzania (TRC) Machibya Masanja ameongeza kuwa Reli ya Kisasa (SGR) inaendelea kuimarisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo nchini huku idadi ya abiria waliohudumiwa tangu kuanza kwa uendeshaji wa huduma hiyo Julai ikifikia milioni 7.6 hadi Septemba mwaka huu huku Huduma hiyo ikiwa inalenga kurahisisha usafiri, kupunguza muda wa safari na kuongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi nchini.

Sanjari na hayo Kituo cha Bahi kilichopo katika kipande cha pili cha mradi wa SGR cha Morogoro–Makutupora ni miongoni mwa vituo muhimu vinavyohudumia abiria na mizigo ambapo Kituo hicho kina jukumu la kuwaunganisha watumiaji wa reli ya kisasa na reli ya zamani (MGR) kupitia shughuli za uhamishaji wa mizigo.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com