KAULI YA WAKILI WA MWANAMUZIKI MKONGWE BABU SEYA NA PAPII KOCHA BAADA YA KUACHIWA HURU




Wakili Mabere Marando aliyekuwa akimtetea mwanamuziki mkongwe nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, amesema uamuzi wa Rais John Magufuli kuwasamehe umekuwa ni ‘surprise’ (jambo la kushtukiza) kwake.


Babu Seya na Papii Kocha ambaye pia ni maarufu kama Mtoto wa Mfalme walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuwabaka na kuwalawiti watoto 10 wa kike ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.


Tayari walishatumikia kifungo hicho kwa miaka 13 na miezi minne.


Wakili Marando ambaye aliwatetea katika rufaa yao ya pili Mahakama ya Rufani alisema uamuzi wa Rais Magufuli umemshangaza na ameupokea kwa furaha kubwa.


Marando ambaye alifanikiwa kuwatoa kifungoni watoto wawili wa Babu Seya, Mbangu na Francis katika rufaa hiyo alisema hakutarajia uamuzi kama huo.


“Asante sana, asante sana, asante sana, namshukru sana Rais Magufuli kuwasamehe, kwa kweli sikutarajia hili. Hii imekuwa ni surpirise, asante sana,” alisema Wakili Marando ambaye alikuwa hajapata taarifa za uamuzi huo hadi alipoulizwa na mwandishi wetu.

Na James Magai, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527