DIAMOND PLATNUMZ AZUNGUMZIA HUKUMU YA LULU JELA MIAKA MIWILI

Mwanamuziki Diamond Platnumz amesema hukumu ya miaka miwili aliyopewa mwigizaji Elizabeth  Michael maarufu Lulu siyo adhabu bali ni mtihani ambao unalenga kumfanya kuwa imara zaidi.

Amesema mwigizaji huyo ambaye leo Jumatatu Mahakama Kuu imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela, amechaguliwa na Mungu kwa kuwa anaamini anao uwezo wa kuhimili mikikimikiki.

Katika mtandao wa Instagram, Diamond anayetamba na wimbo Halleluyah, ameandika:  "Mwenyezi Mungu ameamua kukupa mtihani huu wewe kwa sababu anaamini wewe ni shujaa na imara...pia anaamini wewe ndio msichana pekee unayeweza kuuhimili mtihani huu... hivyo usisononeke, Make him Proud.”

Mbali na Diamond, wasanii wengine wametuma salamu za pole kwa Lulu akiwamo Wema Sepetu, Mboni Masimba, Snura, Dj Choka, Dk Cheni na wengine wengi.

Dk Cheni ambaye amekuwa karibu na Lulu kwa muda mrefu amesema huu ni wakati wa kumuombea Lulu kwa kuwa hakuna anayejua kesho atapata mkasa gani.

Katika mtandao wa Instagram aliweka picha ya Lulu na kuandika: "Tumuombee mtoto huyu kwa kuwa hakuna anayeijua kesho yake,".


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527