Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAVITAKA VYUO KUTOA ELIMU YA AFYA YA AKILI NA USIMAMIZI WA FEDHA KWA WANAFUNZI

Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Stephen Maluka, amevitaka vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya kati kuhakikisha vinaandaa programu maalumu za kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu ustawi wao, ikiwemo elimu ya afya ya akili na usimamizi wa fedha binafsi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa ustawi wa wanafunzi wa vyuo vikuu, Prof. Osward amesema programu hizo zinapaswa kupewa kipaumbele wakati wa utambulisho wa wanafunzi wapya (Orientation), ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanapokuwa chuoni.

Amesema Serikali itatumia matokeo ya ripoti hiyo kama rejea muhimu katika kufanya mapitio ya sera na miongozo ya usimamizi wa ustawi wa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini.

Aidha, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua mwongozo wa kuingiza elimu ya fedha katika mitaala ya vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya kati, ambao tayari umewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya utekelezaji.

Vilevile, amewataka viongozi wa serikali za wanafunzi kuwa mabalozi wa ustawi kwa kuanzisha klabu za majadiliano na michezo, huku akiwahimiza wanafunzi kutafuta msaada wa kitaalamu wanapokabiliwa na changamoto za afya ya akili, msongo wa mawazo na ugumu wa maisha.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya wateja Binafsi CRDB Bank Plc Steaven Adili, amesema benki hiyo imeanzisha huduma na idara maalumu zinazolenga kukidhi mahitaji ya vijana, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu huku akiongeza kuwa afya bora ya akili kwa vijana ni muhimu katika kuongeza ufanisi kazini na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema uwekezaji huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayotegemea sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya utekelezaji wake, akizitaka taasisi nyingine kuwekeza kwa vijana ili kuongeza uzalishaji na tija nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Bloom Wellness Foundation, Sophia Byanaku, amesema baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanakabiliwa na changamoto za kifedha zinazowalazimu kukopa kwa riba kubwa, kuweka vifaa vyao vya shule kama dhamana na wengine kujihusisha na michezo ya kubashiri ili kupata fedha za kujikimu.

Akizungumza kuhusu matokeo ya utafiti uliohusisha wanafunzi 635, Byanaku amesema wanafunzi wengi wanategemea mikopo kama chanzo kikuu cha mapato, hivyo mikopo inapochelewa au kuisha hukosa akiba ya kuwasaidia, hali inayowafanya baadhi kushindwa kumudu mahitaji muhimu kama chakula na malazi.

Amesema changamoto hizo zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu ya fedha na stadi za vitendo kuhusu upangaji wa bajeti na uwekaji wa akiba, akisisitiza kuwa hali hiyo si uzembe wa wanafunzi bali ni matokeo ya kukosa maarifa na njia sahihi za kukabiliana na changamoto za kifedha.

Aidha, amezitaka taasisi mbalimbali kushirikiana katika kutoa elimu ya fedha kwa vijana, akieleza kuwa ripoti hiyo imelenga kuonesha hali halisi ya maisha ya wanafunzi ili kupata suluhisho la pamoja, huku akiishukuru Wizara kwa kuitikia wito huo na CRDB Bank kwa kufadhili mafunzo ya stadi za fedha.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mtafiti, Dkt. Hezron Zakaria Mnditi amesema Wanafunzi saba kati ya kumi, sawa na asilimia 70, wa vyuo vikuu nchini wamebainika kukabiliwa na msongo wa mawazo, huku asilimia 20 wakiripoti kupitia hali ya hofu na wasiwasi wakiwa katika mazingira ya vyuo

Amesema utafiti huo ulilenga kubaini changamoto zinazokabili wanafunzi katika maeneo ya afya ya akili, ustawi wa kisaikolojia na kijamii ili kuweka msingi wa kuandaa afua za kuwasaidia.

Amesema utafiti huo uliangazia changamoto za sonona, mfadhaiko, hofu na wasiwasi, pamoja na masuala ya ukatili, matumizi ya vifaa vya teknolojia ya mawasiliano, upatikanaji wa milo inayostahili na uwezo wa wanafunzi kukabiliana na changamoto za maisha ya chuo.

Dkt. Mnditi amesema utafiti huo ulihusisha wanafunzi 623 kutoka Chuo Kikuu cha Kampala International na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), pamoja na watendaji wa vitengo vya ushauri nasaha na viongozi wa wanafunzi, ambapo jumla ya washiriki walikuwa 635.

Ameeleza kuwa lengo la kufanya utafiti huo wa awali ni kupata taarifa zitakazosaidia Serikali na taasisi za elimu ya juu kubuni programu na hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuimarisha ustawi wao wawapo vyuoni.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com