Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEMC YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KUPITIA COP31 - ANTALYA, UTURUKI; NOVEMBA 2026


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeimarisha ushirikiano na wadau wa kimataifa kupitia mikutano iliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), jijini Antalya, Uturuki, Novemba 2026.

Akizungumza katika Mikutano hiyo iliyolenga kupanua fursa za upatikanaji wa fedha, utaalamu na teknolojia, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema rasilimali hizo ni kwa ajili ya kulinda mazingira na kuimarisha ustahimilivu wa Tanzania dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo NEMC ndio wajibu wake kuhakikisha hilo linafanikiwa

NEMC pia ilifanya mazungumzo na washirika wa kimataifa, wakiwemo Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (GCF) ambapo ilipongeza kuhuishwa kwa ithibati yake kwa kipindi kingine cha miaka mitano pamoja na kuidhinishwa kwa miradi ya Urejeshaji wa Ziwa Babati na Kujifunza na Kubadilishana Maarifa wa SWAHAT.

Aidha, Baraza liliomba kuharakishwa kwa mapitio ya maandiko ya miradi yenye mahitaji ya takribani dola za Marekani milioni 30, inayolenga sekta ya maji, mifumo ikolojia na shughuli za kiuchumi zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), NEMC ilifuatilia hatua za kuharakisha maandalizi ya mradi wa ustahimilivu wa maeneo ya pwani, ambao andiko lake la awali liliidhinishwa Juni 2024. Katika mazungumzo hayo, Benki ilieleza dhamira ya kuunga mkono mradi huo unaolenga kulinda jamii na mifumo ikolojia ya maeneo ya pwani ya Tanzania Bara na Zanzibar dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile, katika kikao na Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (GCF), mazungumzo yalijikita katika hatua za kuendeleza ushirikiano baada ya NEMC kupata ithibati, hususan maandalizi ya miradi na kuimarisha uwezo wa kitaasisi ili kuwezesha upatikanaji wa fedha za tabianchi.

Katika eneo la kukabiliana na changamoto za uhamaji unaotokana na mabadiliko ya tabianchi, NEMC na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS), kupitia Global Centre for Climate Mobility (GCCM), zimekaribia kukamilisha makubaliano ya kushughulikia masuala ya watu wanaolazimika kuhama au kuhamishwa kutokana na athari za tabianchi. Katika mazungumzo hayo, NEMC ilisisitiza utayari wake wa kuhakikisha miradi itakayotekelezwa inasimamiwa kwa weledi.

Aidha, katika kikao na taasisi ya iFOREST, NEMC ilijadili masuala ya usafiri safi, nishati jadidifu na hatua za kukabiliana na ongezeko la joto katika maeneo ya mijini. Pande hizo zilikubaliana kuanza kwa kufanya utafiti katika maeneo ya Dar es Salaam yanayoathiriwa zaidi na joto, kwa lengo la kubaini maeneo yenye athari kubwa na kupendekeza hatua stahiki. Matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi, kuendeleza miundombinu ya kijani na kutumia teknolojia za upoezaji zinazolinda afya na ustawi wa wananchi.

Sambamba na hilo, NEMC ilifanya mazungumzo na Jukwaa la Taka Sifuri (Zero Waste Forum), yaliyolenga kuendeleza programu ya Baraza ya kupunguza uzalishaji wa taka, kutumia tena bidhaa na kuchakata taka ili kuzibadilisha kuwa rasilimali zenye manufaa.

Katika mikutano hiyo, waliyoambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yusuph Masauni, NEMC imeonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhakikisha fursa za kifedha, kiteknolojia na kitaalamu zinapatikana na kuunganishwa na vipaumbele vya Taifa. 

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi mazingira, kulinda jamii na kuendeleza maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com