Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI BABATI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA UHIFADHI NA MABADILIKO YA TABIA NCHI VIJIJINI

Na Mwandishi wetu, Babati

Wanafunzi 40 wa shule za Sekondari zilizopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge (Burunge WMA) Wilayani Babati mkoani Manyara, wametakiwa kwenda kutoa elimu vijijini kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, utunzwaji wa mazingira na faida za uhifadhi wa Wanyamapori baada ya kupatiwa elimu hiyo katika ziara ya mafunzo waliyofanya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Babati vijijini, Anna Mbogo, ametoa maagizo hayo, Oktoba 25, 2026 wakati akiwapokea wanafunzi hao, walipokuwa wakirejea wilayani Babati, baada ya kukamilika kwa safari ya mafunzo ya siku tano iliyoandaliwa na Taasisi ya Chem chem Association, ambayo imewekeza shughuli za Utalii na Uhifadhi katika eneo hilo.

Mbogo amesema, wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara ni miongoni mwa wilaya nchini, ambazo zinaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi lakini, bado kuna watu hawajuwi athari za mabadiliko hayo, hivyo ni jukumu la wanafunzi hao kushirikiana na walimu wao na wadau wengine, kutoa elimu hiyo ili kusaidia jamii.
"Tunaona misimu ya mvua imebadilika sana, joto limeongezeka na tunatarajia mwaka huu kuwepo na mvua za El- Nino hivyo, nyie wanafunzi mmepewa elimu juu ya mambo haya, ikiwepo utunzwaji wa mazingira tunatarajia mkirudi vijijini mkatoe elimu hii",amesema.

Mkurugenzi huyo, amesema Safari iliyoandaliwa na Chem Chem kwa wanafunzi hao, pamoja na watendaji wa serikali na wazazi itakuwa na manufaa makubwa kama elimu, iliyopatikana itafika kwa watu wengi ili kuendeleza utunzwaji wa mazingira na wanyamapori.

"Nyie mmepata fursa kubwa kutembelea kujifunza Serengeti na Ngorongoro lakini kuna Watanzania wengi hawajapata fursa hiyo na kuna wengine wanalipia fedha nyingi kuipata hii fursa, sasa mkawe mabalozi wazuri kuendeleza uhifadhi na utalii", amesema.

Amesema ziara hiyo, ni sehemu ya utekelezaji maagizo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu, kuhakikisha Uhifadhi na Utalii unaendelezwa nchini,kwani tayari Rais ametangaza Utalii na Uhifadhi kupitia filamu ya The Royal Tours ambayo imesambaa duniani kote.

Mkurugenzi wa Chem Chem Association, Clever Zulu amesema taasisi hiyo na wadau wengine, wameamua kugharamia ziara hiyo ambayo sasa ni mara ya pili kufanyika, ili kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo uhifadhi na Utalii baadae kurejea kutoa elimu.

"Chem Chem tunaamini nyie bado ni watoto mkifahamu vizuri faida ya uhifadhi na Utalii, mtaelimisha wengine na mtarithisha vizazi vijavyo faida za Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori waliopo sasa", amesema.

Afisa Wanyamapori wilaya ya Babati, Christopher Laizer amesema ziara hiyo inafaida kubwa katika kuendeleza uhifadhi na sasa wameongezeka mabalozi ambao watakwenda kutoa elimu na masimulizi mazuri ya faida ya uhifadhi na Utalii vijijini.

Afisa Miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Chem Chem, Napendali Wazoeli aliwashukuru walimu, kampuni ya Utalii ya Kanaga, taasisi za Mkono kwa mkono na Serikali kwa ujumla kufanikisha ziara hiyo ya siku tano ya mafunzo.

Baadhi ya wanafunzi na Wazazi, walioshiriki ziara hiyo, walishukuru Chem Chem na Serikali kwa kufanikisha ziara hiyo na wamejifunza mengi ambayo watayatumia katika maisha yao na kuelimisha jamii.

Wanafunzi Fatuma Shaban na Lulu John, walisema elimu ambayo wameipata wataitumia vizuri kuelimisha wengine, kwani wao wamejifunza mambo mengi kuhusiana na uhifadhi, tabia za wanyamapori, masuala ya mabadiliko ya tabia nchi.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com