Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, ameendelea na kampeni ya Ongea na Kamanda katika Kata ya Bulige, Halmashauri ya Msalala, akiwahimiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu.
Akizungumza na wananchi hao Oktoba 21,2026, Kamanda Magomi amewashukuru kwa juhudi zao za kujenga kituo cha Polisi katika eneo hilo, akieleza kuwa kitakapokamilika kitasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za kipolisi na kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi, huku akisisitiza umuhimu wa kutovumilia vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha vinatolewa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe.
Aidha, Kamanda Magomi amewakumbusha wananchi kuhusu kampeni ya kusalimisha silaha haramu, akieleza kuwa inatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, 2026.
AMEonya kuwa baada ya muda huo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kumiliki silaha haramu.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Bulige wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano katika ujenzi wa kituo hicho na kuomba askari wapangiwe kituoni hapo mapema ili kianze kutoa huduma mara baada ya kukamilika.
Kamanda Magomi pia aMEtembelea eneo la ujenzi kukagua maendeleo ya kazi na kupongeza hatua iliyofikiwa.











TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin