Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DODOMA YAKAMILISHA SAFARI YA KUWA MAKAO MAKUU YA SERIKALI, SAMIA AMKUMBUKA MAGUFULI

Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa hatua muhimu za kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Serikali ni matokeo ya maono ya muda mrefu yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na kuendelezwa na viongozi waliomfuata, akiwemo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Samia amemtaja Dkt. Magufuli kwa namna ya pekee, akimpongeza kwa kusimamia na kuendeleza mpango wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma, hatua aliyosema imechangia kutimiza ndoto ya kuwa na makao makuu ya nchi katikati ya Tanzania.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma, mradi wa kimkakati uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 700 na unaojumuisha majengo ya wizara, taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na miundombinu wezeshi.

Amesema mafanikio hayo hayapaswi kuhusishwa na uongozi mmoja pekee, bali ni matokeo ya mchango wa viongozi mbalimbali walioweka msingi na kuendeleza azma hiyo katika vipindi tofauti vya uongozi wa nchi.

Ameeleza kuwa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma kulilenga kusogeza huduma za umma karibu na wananchi, kurahisisha upatikanaji wake na kupunguza gharama za safari ambazo wananchi walikuwa wakizitumia kufuata huduma katika maeneo mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesisitiza kuwa kuhamia kwa Serikali Dodoma hakumaanishi wananchi kutoka maeneo mengine nchini wanapaswa kusafiri hadi jijini humo ili kupata huduma za Serikali.

Badala yake, amesema Serikali inaendelea kupanua matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili wananchi waweze kupata huduma mbalimbali za umma kwa njia za kidijitali wakiwa katika maeneo yao, bila kulazimika kufika Dodoma.

Uzinduzi wa Mji wa Serikali wa Mtumba ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya utawala na kuweka mazingira bora ya utendaji kazi kwa wizara na taasisi za Serikali, sambamba na kuendeleza nafasi ya Dodoma kama kitovu cha shughuli za Serikali nchini.
















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com