Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIKI YA ELIMU TANGA KUWAPA WANANCHI FURSA ZA KUJIFUNZA NA KUBUNI



Na.Mwandishi Wetu

Wananchi wa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani wanahamasishwa kushiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ubunifu na Ujuzi, itakayofanyika kuanzia tarehe 15 - 24 Agosti 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ili kujifunza, kubadilishana maarifa na kutumia fursa mbalimbali za elimu, ujuzi na ubunifu.

Akizungumza Agosti 14, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Kassim Mchata, amesema maonyesho hayo yatashirikisha taasisi zaidi ya 300 pamoja na wadau wa sekta ya elimu, sayansi na teknolojia. 

Aidha, kutakuwa na mashindano ya ubunifu na ujuzi katika fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, ususi, umeme na mengineyo, ambapo washindi wa kitaifa watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

Mchata ameongeza kuwa wadhamini mbalimbali wakiwemo mabenki wamejitokeza kudhamini miradi ya ubunifu na kuunga mkono wajasiriamali chipukizi.

Kwa upande wake, Prof. Ladislaus Mnyone, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, alisema lengo kuu la wiki hiyo ni kuwaleta pamoja wadau kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kuhusu elimu, ujuzi na ubunifu

Amebainisha kuwa matukio makuu yatakuwa ni maonesho ya teknolojia yanayoonyesha mchango wa sayansi katika sekta mbalimbali, pamoja na kongamano la elimu na ubunifu litakalojadili utekelezaji wa Dira 2050.

Prof. Mnyone amefafanua kuwa kongamano hilo litaangazia nyenzo tano kuu: utafiti na maendeleo, sayansi na ubunifu, teknolojia za kidijitali, nishati, na usafirishaji funganishi.

Kupitia mijadala na maonesho hayo, Wizara inalenga kufanikisha malengo ya taifa ikiwemo kufikia uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, kipato cha wastani cha mtu mmoja kati ya Dola za Marekani 7,000 - 12,000, na ajira zenye staha kwa angalau asilimia 50 ya Watanzania.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com