
WALIMU 328 kutoka shule 10 za Sekondari katika Jiji la Tanga wanapigwa msasa kupitia semina maalumu inayolenga kuwaongezea ujuzi na mbinu za ufundishaji, hatua inayolenga kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa Kidato cha Pili na Nne.

Semina hiyo inaendeshwa na Taasisi ya Tanzania Centre For Education kupitia mradi wa Tanga Yetu, unaofadhiliwa na Foundation Botnar na kutekelezwa kwa kushirikiana na Innovex, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kukuza ufaulu katika shule za Jiji la Tanga.
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nguvumali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education Yusuf Ogutu alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa semina zilizolenga kuwajengea uwezo walimu katika masomo mbalimbali.

Alisema katika hatua hiyo walimu wa masomo ya Historia, Jiografia, Business Studies na Bookkeeping wamepatiwa mafunzo, huku awali semina ikiwa imefanyika katika Shule ya Sekondari Kihere kwa walimu wa Civics, Kiswahili, Kiingereza, Historia ya Tanzania na Maadili.
Ogutu alisema mpango huo unalenga kuhakikisha walimu wanakuwa na uelewa na lugha moja katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi na hatimaye kuboresha ufaulu.
“Tunawapatia walimu maarifa na mafunzo, pamoja na kuwawezesha gharama za usafiri kutoka walikotoka na kurejea. Hii ni sehemu ya mpango mpana wa kuhakikisha kampeni ya kukuza ufaulu katika Jiji la Tanga inafikia malengo,” alisema.

Alisema kampeni hiyo inatekelezwa kwa hatua mbalimbali, ambapo awamu ya kwanza iliwahusisha wanafunzi, hatua ya pili ni walimu na awamu inayofuata itawahusisha waratibu wa elimu ngazi ya kata, maafisa elimu wa wilaya pamoja na kamati za malezi na wazazi.
Kwa mujibu wa Ogutu, mpango huo unalenga kuwafanya wadau hao kuwa na uelewa unaofanana katika kuhakikisha wanashirikiana kutafuta suluhisho la changamoto zinazoathiri ufaulu wa wanafunzi.
Alisema hadi sasa walimu 85 tayari wamefikiwa kupitia mafunzo hayo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka hadi kufikia walimu 100 katika awamu inayoendelea, kabla ya kukamilishwa kwa mafunzo ya walimu wa masomo ya sayansi.

Ogutu alisema jumla ya walimu 328 katika shule 10 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo, ambao unalenga kutoa mchango katika kuboresha matokeo ya wanafunzi wa Jiji la Tanga.
Wakufunzi kutoka shule bora
Aidha, alisema walimu wanaopatiwa mafunzo hayo wanafundishwa na wakufunzi wenye uzoefu kutoka baadhi ya shule zilizofanya vizuri kitaifa, hatua inayolenga kuwapatia mbinu bora za ufundishaji.
Alizitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni Mzumbe, Marian Boys na Feza Boys, ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

Alisema pia kuna wakufunzi kutoka Canossa pamoja na shule mbalimbali za Serikali zilizowahi kufanya vizuri kitaifa.
“Tunawaamini sana walimu kwa sababu wao ndiyo injini ya matokeo. Ukiwapiga msasa walimu na kuwaongezea uwezo, unakuwa umeweka msingi mzuri wa kuboresha ufaulu wa wanafunzi,” alisema.

Alisema katika semina hizo walimu wanapata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali za ufundishaji, ikiwemo mada ambazo zimekuwa zikiwasumbua, ili kupata ufumbuzi na kuhakikisha wanakuwa na uelewa unaofanana katika ufundishaji.
Alisema kupitia mpango huo, matarajio ni kuona walimu wakiboresha namna ya kufundisha na wanafunzi wakipata uelewa mzuri wa masomo, jambo litakalosaidia kuongeza ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Pili na Nne.

Mpango huo ni sehemu ya juhudi za Tanga Yetu za kuwaunganisha wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu katika kutafuta njia za kuboresha kiwango cha ufaulu katika shule za Jiji la Tanga.


Social Plugin