HIVI NDIVYO SUGU NA MASONGA WALIVYOWASILI MAHAKAMANI KUSIKILIZA HATMA YA KESI YAO

Ulinzi umeimarishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambako itatolewa hukumu ya kesi inayomkabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Katika eneo la mahakama wapo askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiimarisha ulinzi nje ya jengo. Tayari washtakiwa wameshafika mahakamani.

Mahakama leo Februari 26,2018 inatoa hukumu ya kesi ambayo Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Wawili hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hukumu inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite aliyesikiliza kesi hiyo. Upande wa mashtaka na wa utetezi ulikamilisha ushahidi Februari 9,2018.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.

Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa, hivyo sasa wanawakilishwa na Peter Kibatala.

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527