JINSI MBUNGE GODBLESS ALIVYOTIBUANA NA MKUU WA MKOA WA ARUSHA MBELE YA WAFADHILI

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, jana alikuwa katika wakati mgumu baada ya  kuzomewa na wananchi wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto   mjini Arusha.

Tukio hilo lilitokea wakati kiongozi huyo alipozungumzia mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo na kudaiwa kupotosha ukweli wa mradi huo.

Katika maelezo yake, Gambo alisema eneo la hospitali hiyo lilitolewa na familia ya Nyaga Mawalla, jambo ambalo   wananchi walilipinga wakishirikiana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).

Hospitali hiyo itakayogharimu Sh bilioni tisa, inajengwa kwa wafadhili ambao ni Taasisi ya Maternity Afrika, Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF)  na Mbunge   Lema.

Kabla mkuu huyo wa mkoa hajazomewa, alipewa nafasi ya kuzungumza na ndipo alipoeleza jinsi familia ya Mawalla ilivyotoa eneo hilo.

Wakati akitoa kauli hiyo, Lema ambaye alikuwapo mahali hapo, alisimama na kupaza sauti akisema, “mkuu wa mkoa anapotosha ukweli wa mradi huu”.

Hatua hiyo ya Lema  kulalamika kwa sauti, iliwafanya wananchi nao  kumzoea Gambo huku baadhi yao wakimtuhumu kuingiza siasa katika shughuli za maendeleo.

Kutokana na zomeazomea hiyo,  polisi waliokuwapo mahali hapo  wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi, walilazimika kusogea eneo la meza kuu huku wengine wakimzunguka Gambo aliyekuwa akiendelea kubishana na Lema kuhusu ukweli wa mradi wa hospitali hiyo.

“Huyoo, acha kupotosha ukweli wewee, usilete siasa kwenye maendeleo, huyooooo,” zilisikika sauti za wananchi kutoka upande wa pili wa meza kuu huku Lema naye akisikika akihoji kwa nini mkuu huyo wa mkoa alikuwa akisema uongo.

Katika hotuba yake ambayo pia ilikatishwa baada ya kutokea kelele hizo, Gambo aliishukuru familia ya marehemu Mawalla kwa kile alichosema ilitoa eneo hilo na kuwatafuta wafadhili wa kujenga hospitali hiyo.

“Hili wazo lilikuwa ni la familia ya Mawalla kwa sababu  ardhi ni mali yao na walikuwa na maono ya kujenga hospitali hii.

“Kwa hiyo, Serikali itakuwa pamoja nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnafanikiwa,” alisema Gambo huku akizomewa na wananchi.

Wafadhili kutoka Ulaya waliokuwa kwenye uzinduzi huo, walijikusanya makundi na kumkumbatia Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maternity Afrika, Andrew Brown, wakimpa pole kwa kile kilichotokea.

Hata hivyo, baadhi ya wafadhili hao walianza kulia wakionyesha ni kwa kiasi gani hawakuridhishwa na mvutano kati ya mkuu wa mkoa, mbunge na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi huo, Lema alisema mkuu huyo wa mkoa alifanya makosa kuupotosha umma kuhusu mradi huo.
“Mkuu wa mkoa alitakiwa kufika saa 4.00 asubuhi lakini hakuonekana kwa madai kwamba asingeweza kuja kama mimi nipo.

“Ilipofika saa saba kasoro bila kumuona, nikampigia simu Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi kumweleza suala hili, naye akampigia simu Katibu Mkuu Tamisemi.

“Inavyoonekana Tamisemi walimpigia simu mkuu wa mkoa ndipo akaamua kuja akiwa amechelewa.

“Kwa hiyo, kilichofanyika hapa kinaonyesha aina ya viongozi walioaminiwa na Rais John Magufuli wamsaidie kuongoza nchi.

“Wafadhili walimualika kuipa heshima Serikali, lakini hakuonekana hadi alipopewa maagizo.

“Kwa faida ya wasiofahamu ni kwamba mimi kupitia ArDF ndiyo tuliotafuta ardhi kwa marehemu Nyanga Mawalla.

“Kibaya zaidi, alipofika hapa akaagiza ratiba ibadilishwe mimi nisizungumze kwa sababu anazozijua yeye.

“Ushahidi wa ratiba hiyo ni kwamba, ilipangwa azungumze mtendaji mkuu wa Maternity Afrika, kisha mkurugenzi wa ArDF, baadaye mimi mbunge pamoja na Mawalla kutoa historia ya mradi na mwisho mkuu wa mkoa.

“Lakini, ratiba hiyo haikufuatwa na badala yake alifanya anavyojua yeye  mradi tu nisizungumze.

“Sasa, hivi unawezaje kuwalazimisha  Maternity Afrika wasinilete mimi wakati kwenye mkataba wa hili eneo mimi na ArDF ndiyo wasimamizi wa mradi?” alihoji Lema.

Mwenyekiti wa ArDF, Elifuraha Mtoi, alisema Taasisi ya ArDF kwa kushirikiana na Lema ndiyo waliofanikisha mradi huo.

“Hizi ni jitihada binafsi za ArDF kwa sababu  baada ya kupata wafadhili, tuliwaunganisha na Mawalla Trust ambao ndiyo wamiliki wa maeneo haya.

“Kwa hiyo, kilichofanywa na mkuu wa mkoa kimetufedhehesha mbele ya wafadhili,” alisema Mtoi.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Maternity Afrika (Brown), alisema fedha za ujenzi wa hospitali hiyo zitatokana na michango mbalimbali ya wafadhili na sadaka kutoka makanisani.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa ambaye pia ni mmoja wa waaanzilishi wa Taasisi ya ArDF, alimtangaza Gambo kama adui wa maendeleo mkoani Arusha.

KATIBU MKUU WA CHADEMA ALAANI TUKIO LA MKUU WA MKOA KUMZUIA MBUNGE GODBLESS LEMA KUWEKA JIWE LA MSINGI,DR SLAA NAYE AFUNGUKA

Nimesikitishwa sana na kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuvuruga sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya huduma za mama na mtoto.


Si tu kwamba ameonyesha kukosa staha kwenye jamii, pia ameonyesha kutounga mkono mahitaji ya nchi na dunia nzima "hasa kwa mahitaji ya akina mama na watoto"

Nalaani tabia hizi za kihuni zisizo na tija kwa Taifa. Ikumbukwe tu kwamba; mwanzo wa ngoma ni lele. Tabia ya Mkuu huyu wa mkoa inajenga chuki na yaweza kuleta machafuko yasiyo ya lazima. Mtu wa hivi hafai kabisa katika jamii

Tumpinge!
Katibu Mkuu Chadema Dr Vicent Mashinji.

Wakati huo huo naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilibard Slaa naye ametoa maoni yake kuhusiana na tukio hilo.
Ameandika kwenye kupitia maoni wake wakati akichangia mjadala huo kuhusiana maoni kuhusu tukio hilo.
Watanzania, Na hasa Viongozi wanaoendekeza propaganda, kumbukeni " Historia haiwezi kufungiwa kwenye chupa", hata ukijaribu kuifungia chupa italipuka na itakurarua uso. Jihadharini na propaganda za kitoto. Uongozi ni kusimamia ukweli na kuwapeleka unaowaongoza kwenye mwanga siyo kwenye giza. Viongozi wa aina hii, wasio na aibu, kudanganya umma hadharani hawafai.Dr Slaa
Dr Slaa anaandika!

Mrisho Gumbo,
Naamini hii ID ni ya kwako na hasa kwakuwa kwenye post unaonekana ukizungumza, napata uhakika kuwa ni wewe.

1) Mkuu wa Mkoa, nakuheshimu kwa kuwa cheo chako ni kikubwa sana. Hata hivyo, ulichokifanya leo na " propaganda unazopiga zimenifanya nikudharau na kukupuuza. Ningeliweza kuishia katika kukudharau na kukupuuza, lakini

2) Aibu uliyoiletea Taifa letu leo, inanifanya " nipige kelele" kuwa " siasa za maji taka siyo wakati wake huu.
a) Mhe.Mrisho Gumbo, wewe kama Mkuu wa Mkoa unayo au mamlaka au vyombo vya dola kukusaidia kufanya utafiti wa maana kuliko aibu kubwa uliyoiletea Taifa letu mbele ya Wahisani/ Wafadhili wetu kupitia Maternity Africa. Hukufanya hivyo, umeamini propaganda kuliko busara na hekima. Kwa hilo siwezi kukusamehe wala kukuheshimu pamoja na cheo au vyeo vyote ulivyonavyo.

b) Mrisho Gumbo, ungelikuwa wa busara iwapo ungelimwomba kiongozi au mwakilishi wa ADF ( ulikuwa na uwezo wa kujua ADF ni nani na historiaya yake ni ipi- kwa kupenda propaganda hukufanya hivyo) au Mwakilishi wa Maternity Africa hasa Happy ( ambaye alisaini pia barua ya kukualika kuwa mgeni rasmi, au hata Mhe. Mbunge Lema ambaye kimsingi ndiye chimbuko la upatikanaji wa Ardhi hiyo kutoka kwa Marehemu Advocate Mawala ( Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi), na pia chimbuko la Upatikanaji mradi kutoka kwa wafadhili wetu. Kutokupenda kushauriwa na hao wenye kujua mradi imekufanya "kuonekana ****" na " mwongo" kwa kuwa historia haifutwi kwa " propaganda za jukwaani". Lakini kwa bahati mbaya athari ya propaganda imeenda mpaka kuichafua Taifa letu kwa wahisani. Ujenzi ndiyo kwanza unaanza. Umeombwa kufanya "Ground Breaking ceremony", unadhani wawakilishi wa wahisani na hasa kule kwenye chimbuko la fedha wanapata picha gani ya Taifa letu.

c) Mrisho Gumbo, busara na hekima ya kawaida ingelikuwezesha kuelewa barua ya mwaliko ambayo imesisitiza mara mbili hivi, kuwa wahusika ni taasisi isiyojihusisha na siasa. Wakasema mradi kwa muda sasa umekumbwa na matatizo yenye sura ya kisiasa. Ulipaswa kutafakari, kutafiti na kutafiti njia makini zaidi ya kuona wakina mama wajawazito, wenye fistula na watoto wachanga hawakosei au hata hawacheleweshewi kupata huduma hiyo kwa sababu za kipuuzi tu. Eti unasoma historia! Unsijua historia au unaota ndoto! Nimepiga kelele kwa kuwa ninaijua vizuri hiyo historia A to Z. Sikuambii ungeliniuliza, lakini wapo kwenye kikao hicho ambao wasingelihitaji kuisoma bali kuitoa kichwani historia hiyo, tangu kupatikana kwa Ardhi, mchakato wa kuchora ramani, kuisajili na kupata vibali vyote vya Kituo hicho cha Afya( japo kwa kweli ni hospitali ( inaitwa kituo cha Afya tu kwa. Sababu za kisheria).

3) Mrisho Gumbo, kwa hili Watanzania wa Arusha na wote wenye kujua ukweli hatutakusamehe kwa aibu uliyotupatia, na kujenga misingi ya kutufungia miradi mingine kwa wahisani wetu. Kama una chembe dogo la busara:
a) Utakaa chini na kutafakari umekosea wapi. Ikiwa lazima
b) uwe na unyenyekevu uwaite wahusika wote ofisini kwako waombe wakupe " historia kamili" na wakupe mchakato mzima mpaka kufikia siku hii muhimu ya " Ground Breaking ceremony( uzinduzi wa Kazi ya ujenzi).

c) Ukipata Taarifa kamili, uwe na unyenyekevu, acha kiburi. Kiburi hakikusaidii wala haitasaidia jamii unayopaswa kuwatumikia ( unless una malengo tofauti). Kwa unyenyekevu mkubwa Waombe msamaha Wahisani wetu kwa kuwaingiza katika " siasa ya Arusha" ambayo hawahusiki nayo; awaombe msamaha wakina mama, watoto na jamii ya Wananchi wa Arusha wapenda maendeleo kwa kuwachafua na kuwaletea vurugu kiasi cha kuifanya Arusha ionekane kila leo ni mahali pa vurugu, kumbu vurugu husababishwa na viongozi wasiotumia busara na hekima. Uongozi ni busara na hekima siyo mabavu wala nguvu ya mamlaka.

Nimeyasema haya kuuchungu mkubwa. Mimi siko kwenye siasa, na wala sina interest na siasa. Siangalii uso w a mtu. Kama ambavyo niliaga kuwa " Nastaafu Party Politics, lakini nitapiga kelele pale maslahi ya Taifa langu yanavyokanyagwa" nitakuwa mwendawazimu kunyamaza wakati mradi wa Tshs Takriban 9 Billioni unahatarishwa na upuuzi na uzembe wa kiongozi mnoja mwenye kuendekeza propaganda zisizo na msingi.

Nawaomba sana Radhi wahisani wetu. Mtuvumilie siyo kwa ajili yetu bali kwa ajili ya kina mama na watoto walengwa wa huduma itakayotolewa na " Kituo cha Mama na Mtoto" ( propaganda ya Hospitali ya mke wa Lema zipuuzeni). Happy, umevumilia mengi katika miradi mingi uliyofadhili na kuisimamia. Usirudi nyuma. Timiza ndoto yako iliyoanza katika umri mdogo sana.

Matunda yanaonekana pamoja na vikwazo vya mara kwa mara vya wapinga maendeleo. Viongozi, " Tenganisheni siasa na Maendeleo" Watumikieni Watanzania bila kuangalia nyuso zao, mrengo wao. Siasa ni sayansi na siasa sayansi ni utumishi.

By Dr Slaa.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527