Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WEREMA: HATUNA MUDA WA KUVURUGA AMANI, VIJANA TULINDE UTULIVU WA NCHI

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Benson Werema, amewataka vijana kuendelea kuwa walinzi wa amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwepo mazingira ya amani na mshikamano.

Werema ametoa kauli hiyo leo Juni 24, 2026 wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Shinyanga, ambapo amesema vijana wana jukumu kubwa la kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani licha ya changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Amesema UVCCM itaendelea kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

"Naomba tutunze amani ya nchi. Hatuwezi kufanya maendeleo bila amani. Tuwaambie wale wenye nia ya kuvuruga amani kuwa sisi tunahitaji amani. Sisi vijana hatuna muda wa kuvuruga amani, bali tuna jukumu la kushiriki katika maendeleo ya taifa," amesema Werema.

Ameeleza kuwa jukumu la vijana si kushiriki migogoro na malumbano yasiyo na tija, bali kuwa sehemu ya suluhisho kwa changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla.

Werema amesema vijana wa CCM wataendelea kuwa mabalozi wa amani kwa kuhubiri mshikamano, upendo na uzalendo katika maeneo yao.

"Tutaendelea kuhubiri amani na kuhamasisha vijana wenzetu kushiriki katika shughuli za maendeleo. Taifa letu linahitaji utulivu ili wananchi waendelee kufanya kazi na kujiletea maendeleo," amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa vijana wana wajibu wa kulinda mafanikio yaliyopatikana kutokana na amani na utulivu uliopo nchini kwa kushirikiana na vyombo vya dola na viongozi mbalimbali katika kuhakikisha sheria na taratibu za nchi zinaendelea kuheshimiwa.

Werema amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Soma pia : RC MBONI MHITA: UVCCM NI TANURU LA KUANDAA VIONGOZI WA TAIFA

 UVCCM SHINYANGA: TUSIHANGAIKE NA MATUSI YA WAPINZANI MTANDAONI, TUWAJIBU KWA MATOKEO YA KAZI

WEREMA: HATUNA MUDA WA KUVURUGA AMANI, VIJANA TULINDE UTULIVU WA NCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com