Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amepokea viti mwendo 60 vyenye thamani ya Shilingi milioni 65 vilivyotolewa na Taasisi ya Wheelchair Foundation ya Marekani kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi viti hivyo iliyofanyika Julai 8, 2026 jijini Arusha, Makalla amesema msaada huo utaongeza uwezo wa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, huku akiishukuru Wheelchair Foundation kwa kuendelea kugusa maisha ya Watanzania wenye mahitaji maalumu.
Aidha, ametoa pongezi kwa Chem Chem Association kwa kuratibu ushirikiano huo uliowezesha msaada huo kuwafikia wananchi wenye uhitaji.
Makalla amesema ujio wa viongozi wa Wheelchair Foundation kutoka Marekani ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa katika kusaidia jamii, akiwahakikishia usalama katika kipindi chote watakachokuwa nchini pamoja na kuwakaribisha kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Arusha.
Amesema Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu na ukarimu, hali inayowavutia wageni kutoka mataifa mbalimbali, hususan Marekani ambayo ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuleta watalii nchini.
Pia amewataka wageni hao kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza Tanzania kimataifa baada ya kushuhudia vivutio na mazingira mazuri yaliyopo nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Wheelchair Foundation, David Behring, amesema taasisi hiyo imejikita katika kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapatia viti mwendo vinavyowapa uhuru wa kutembea, heshima na fursa ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya kila siku.
Amesema viti hivyo vitawawezesha wanufaika kufika shuleni, maeneo ya kazi na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila utegemezi mkubwa wa watu wengine.
Naye Mkurugenzi wa Miradi wa Chem Chem Association, Aurelia Klasarah, amesema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Wheelchair Foundation utaendelea ili kuhakikisha watu wengi zaidi wenye uhitaji wanapata msaada wa vifaa vya usaidizi.
Kwa upande wake, Mtunza Hazina wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Arusha, Ndekirwa Palangyo, ameishukuru Wheelchair Foundation kwa msaada huo, akisema utaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wanufaika na kuongeza matumaini kwa watu wengi wenye ulemavu mkoani humo.
Miongoni mwa wanufaika wa viti mwendo, Farida Mwinyi mwenye umri wa miaka 34 kutoka Njiro amesema msaada huo utabadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa kutokana na changamoto za utembeaji alizokuwa akikabiliana nazo nyumbani.
Amesema mazingira ya nyumbani kwake hayakuwa rafiki kwa mtu mwenye ulemavu, kwani wakati wa kwenda msalani au kutoka sebuleni kuelekea chumbani alilazimika kubebwa na mtu mwingine.
Kwa upande wake, mnufaika mwingine, Sebastian Gabriel, mwenye umri wa miaka 50 mkazi wa Kisongo, Arusha, amesema kabla ya kupata kiti mwendo alikuwa akitumia magongo ambayo yalikuwa yakimsababishia maumivu na kumfanya ashindwe kutembea kwa urahisi.
Amesema kupokea kiti mwendo kutamwezesha kusafiri kwa urahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kumrahisishia shughuli zake za kila siku.
Aidha, amesema kuwa anajishughulisha na kilimo, hivyo kiti hicho kitamsaidia kufika shambani na kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato bila vikwazo vikubwa vya usafiri.






Social Plugin