Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MBONI MHITA: UVCCM NI TANURU LA KUANDAA VIONGOZI WA TAIFA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza katika kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 Blog

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ni tanuru muhimu la kuandaa viongozi wa taifa na nguzo ya kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi.

Mhita ametoa kauli hiyo leo Juni 24, 2026 wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la UVCCM Mkoa wa Shinyanga, ambapo amewataka vijana kutumia nafasi waliyopewa ndani ya jumuiya hiyo kujifunza misingi ya uongozi, uzalendo na uwajibikaji ili wawe viongozi bora wa sasa na baadaye.

"Jumuiya ya Vijana ni tanuru la kuoka viongozi. Hapa ndipo viongozi wengi wanapoandaliwa na kujengwa. UVCCM ni hazina ya viongozi wa taifa letu," amesema Mhita.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwawezesha vijana kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi.

"Dkt. Samia ni kiongozi anayewapenda vijana. Ni lazima vijana wawe na nidhamu. UVCCM ni jeshi la CCM ambalo lipo tayari kukitetea chama na kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema.

Mhita amesema Mkoa wa Shinyanga umeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa serikali katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, ambapo zaidi ya shilingi trilioni 1.7 zimeelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Samia, Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na imeendelea kuboresha huduma kwa wananchi," amesema.

Aidha, amewataka vijana kuwa mabalozi wa maendeleo kwa kuwaelimisha wenzao kuhusu fursa zinazotolewa na serikali, hususan mikopo ya vijana inayotolewa kupitia halmashauri.

"Vijana waendelee kufuatilia na kutumia fursa zilizopo. Serikali imetoa fursa nyingi kwa vijana kuanzia ngazi ya halmashauri. Ninyi ndiyo wasemaji na watetezi wa vijana, waelekezeni namna ya kunufaika na fursa hizo na wahamasisheni kuchukua mikopo na kuirejesha kwa wakati," amesema.

Mhita pia amewapongeza vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwa nidhamu, ushiriki wao katika shughuli za chama na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, akisema juhudi hizo zimeendelea kuimarisha chama na kuongeza idadi ya wanachama wapya.

"Nawapongeza vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwa nidhamu yenu, kwa kufanya ziara na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mnaifanya CCM iendelee kuwa hai na kuendelea kupata wanachama wapya," amesema.

MWISHO. Kwa upande wa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Benson Werema, amesema vijana wa CCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutangaza mafanikio ya serikali na kusikiliza changamoto za wananchi badala ya kutumia muda mwingi kujibizana na wapinzani kwenye mitandao ya kijamii. Amesema jukumu kubwa la vijana ni kuwaunganisha wananchi na fursa za maendeleo pamoja na kushiriki katika utatuzi wa kero zinazowakabili katika maeneo yao.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amewataka vijana wa UVCCM kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano na nidhamu ndani ya chama huku wakijiepusha na makundi yasiyo na tija. Amesema vijana wanapaswa kujiandaa kuwa viongozi wa baadaye kwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu taratibu za chama na kuendelea kuwa mfano mzuri katika jamii.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com