Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JOWUTA YAKUTANA NA WAZIRI RIDHIWANI, KAMISHNA WA KAZI KUJADILI CHANGAMOTO ZA WANAHABARI

Na Mwandishi Wetu – DODOMA

VIONGOZI wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) wamekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, pamoja na Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, kujadili changamoto zinazowakabili wanahabari nchini, hususan mikataba ya ajira na mazingira bora ya kazi.

Kikao hicho kilifanyika Agosti 21, 2025 jijini Dodoma katika Ofisi ya Waziri Kikwete na kuhudhuriwa na viongozi wa JOWUTA pamoja na watendaji wa wizara.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kikwete alisema wizara yake haitaridhika kuona wanahabari wengi wakifanya kazi bila mikataba na katika mazingira duni.

“Nimewaita hapa tuzungumze kuhusu changamoto zinazowakabili. Mimi binafsi nazifahamu na tunataka kuzitafutia suluhisho. Hali hii haiwezi kuendelea,” alisema Ridhiwani.

Alisisitiza kuwa ni lazima kila sekta nchini ifuate sheria za kazi zilizopo na kuonya tabia ya baadhi ya waajiri kuendesha mambo kwa ujanja ujanja hali inayowaathiri wafanyakazi wanapostaafu au wanapopatwa na matatizo.

Aidha, Waziri huyo alisema anafahamu wanahabari wengi hawana mikataba ya kazi na wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo lazima zifike mwisho, akibainisha kuwa sheria ya kazi ni moja kwa wafanyakazi wote na inapaswa kuzingatiwa katika sekta zote.

“Kama tulivyozungumza Arusha, tulikubaliana leo kukutana tena hapa na Kamishna wa Kazi akiwepo ili kuona ni jinsi gani tunaweza kusaidia wanahabari kufanya kazi katika mazingira bora. Naomba kila mtu aende kutekeleza yale yanayomuhusu tuangalie njia ya kupitia yenye maslahi kwa wote,” alisema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kazi Suzan Mkangwa alisema ofisi yake ipo tayari kushirikiana na JOWUTA kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanahabari.

“Tunaweza kufanya ukaguzi lakini sekta yenu ina changamoto kadhaa za kimfumo ikiwemo utaratibu wa wanahabari wanaolipwa kwa kazi moja moja (correspondent/freelance) au wenye mikataba ya muda (retainer). Huu utaratibu ni mgumu na unapaswa kuondoka ili tuwe kwenye mfumo mmoja kama sekta zingine,” alisema.

Mkangwa aliongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi mara kwa mara na mara nyingi hukuta mikataba ya walio kwenye ajira rasmi pekee, jambo linalofanya iwe vigumu kubaini makundi mengine ya wanahabari. Alitoa wito kwa JOWUTA kushirikiana na ofisi yake ili kupata taarifa sahihi zitakazowezesha kuchukua hatua stahiki.

Vilevile, alisema ofisi yake itaendelea kutoa elimu ya sheria za kazi kwa wanahabari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza kwa niaba ya JOWUTA, Mwenyekiti wa chama hicho Mussa Juma aliomba Serikali kusaidia wanahabari kufanyakazi katika mazingira bora na kuhakikisha sheria za kazi zinafuatwa.

Amesema zaidi ya asilimia 80 ya wanahabari nchini wanafanyakazi bila mikataba ya kisheria, bima ya afya wala mifuko ya pensheni, hali iliyodumu zaidi ya miaka 10.

“Tunakuomba sana Kamishna usaidie sekta hii, ili waajiri wazingatie sheria za kazi na pia tunaomba ukaguzi wa mara kwa mara katika vyombo vya habari,” alisema Juma.

Awali, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya aliishukuru Serikali kupitia Bodi ya Ithibati Tanzania (JAB) kwa kuhakikisha wanaofanyakazi katika vyombo vya habari ni wale wenye sifa za kitaaluma. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa juhudi hizo kuendana na maboresho ya maslahi ya wanahabari, ikiwemo kupewa mikataba, bima na stahiki nyingine.

“Kwa sasa kila kukicha kuna michango ya wanahabari wagonjwa kwani wengi hawana bima wala hawapo kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Tunaomba nguvu hii iliyooneshwa na JAB ionekane pia kwa Kamishna wa Kazi katika eneo la mikataba,” alisema Msuya.

Kwa upande wake, Mweka Hazina wa JOWUTA, Lucy Ngowi alisema sekta ya habari inapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma ili kuhakikisha wanahabari wananufaika na mchango wao mkubwa kwa nchi.

Alisema waandishi wa habari ni nguzo muhimu katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele kama makundi mengine ya wafanyakazi.

“Tunaposema sekta inachangia kwenye pato la taifa, ni vema ikaonekana kivitendo. Sekta hii ya habari yenye zaidi ya watu 30,000 mchango wake bado ni mdogo, lakini iwapo sheria zitafuatwa mchango wetu utaonekana kila mwaka kama sekta za utalii, uvuvi, ujenzi na kilimo,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com