Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Mabula Magangila, amekabidhi magodoro kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Ikinda walioweka kambi shuleni kwa ajili ya maandalizi ya mitihani yao ya mwisho, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu.
Mhe. Magangila ametoa msaada huo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea hali ya wanafunzi hao waliokuwa wakilala katika mazingira yasiyoridhisha, jambo lililomgusa na kumfanya kuchukua hatua ya kuwapatia magodoro ili waweze kupata mapumziko bora na kuendelea na masomo yao kwa utulivu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magodoro hayo, Mhe. Magangila amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kufikia ndoto zake kutokana na changamoto za mazingira ya kujifunzia.
"Nilipofika hapa na kuona hali ambayo watoto wetu wanapumzika, niliguswa sana. Elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa letu, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kupumzika. Magodoro haya ni mwanzo tu wa jitihada za kuendelea kuboresha shule hii," amesema Mhe. Magangila.
Mbunge huyo aliongeza kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kutatua changamoto zinazokabili shule hiyo, ikiwa ni pamoja na kuifungia mfumo wa umeme wa jua ili kuwawezesha wanafunzi kujisomea nyakati za usiku wakati jitihada za kuifikishia huduma ya umeme kupitia Mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zikiendelea.
"Ninawaahidi wanafunzi wa Ikinda kuwa nitafunga mfumo wa umeme wa jua hapa shuleni ili muweze kusoma usiku bila changamoto. Wakati huo huo, nitaendelea kufuatilia kuhakikisha huduma ya umeme wa REA inafika hapa. Tunataka kuona shule hii inafanya vizuri zaidi na kuwa mfano wa mafanikio katika Jimbo la Msalala," amesisitiza.
Naye Diwani wa Kata ya Ikinda, Mhe. Matilda Musoma, amesema kuwa licha ya Shule ya Sekondari Ikinda kuwa mpya, imeendelea kufanya vizuri kitaaluma pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi na walimu.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Msalala, Sostenes Luhende, amewataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kuongeza juhudi katika masomo yao ili kuendelea kufanya vizuri na kuiletea shule heshima kupitia matokeo bora.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ikinda, Leonard Joseph, amesema kuwa uamuzi wa kuwaweka wanafunzi kambini ulitokana na kubaini kuwa wanafunzi wengi wanapokuwa nyumbani hupata muda mchache wa kujisomea, hali inayoweza kuathiri kiwango cha ufaulu, huku akibainisha kuwa shule hiyo bado haina mabweni.
Baadhi ya wanafunzi walionufaika na msaada huo wameeleza shukrani zao kwa Mbunge huyo, wakisema magodoro hayo yatawapa mazingira bora ya kupumzika na kuongeza ari ya kujisomea kuelekea mitihani yao ya mwisho.



Social Plugin