Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na Wakili Julius Mtatiro (Mkuu wa wilaya ya Shinyanga) imefanikiwa kumkamata Bundala Mashiku (24), mkazi wa Kijiji cha Lyabukande, kwa tuhuma za kumuoa mwanafunzi wa Kidato cha Tano ambaye jina lake limehifadhiwa.

Bundala anadaiwa kumuoa mwanafunzi huyo kwa makubaliano ya kulipa mahari ya Shilingi Milioni 4.5, ambapo kiasi hicho kilitarajiwa kulipwa ifikapo Agosti 5 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Wakili Mtatiro amesema mwanafunzi huyo alikuwa amechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Kili iliyopo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, lakini wazazi wake walifanya uamuzi wa kumuoza kwa familia ya Mashiku Sylivesta ili asiendelee na masomo.

Mtatiro amesema Serikali haitavumilia kuona vitendo vya uozeshaji wanafunzi vikiendelea, huku akieleza kuwa Bundala pamoja na baba yake mzazi, Mashiku Sylivesta, wataendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama kwa ajili ya uchunguzi kabla ya kufikishwa mahakamani endapo watapatikana na makosa.

“Natangaza vita kwa wazazi ambao wamewaozesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka huu. Tunaendelea na msako wa kila familia kuhakikisha wanafunzi wote wanakwenda shule ili kutimiza ndoto zao,” amesema Mtatiro.

Amewataka wazazi kuacha tamaa ya mali kwa kuwaozesha watoto wao, akisisitiza kuwa sheria ipo na itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Mashiku Sylivesta amesema hakufahamu kuwa binti huyo alikuwa bado mwanafunzi, akieleza kuwa aliamini alikuwa amemaliza Kidato cha Nne mwaka jana.

Amesema familia ilikubaliana na mahari ya Shilingi Milioni 3 ambayo ilipaswa kulipwa Agosti 5 mwaka huu, huku kiasi kingine cha Shilingi Milioni 1.5 kikitarajiwa kulipwa mwaka 2027.

“Kijana wangu alichumbia mke akamleta nyumbani, familia tukakaa na kukubaliana kulipa mahari hiyo. Sikujua kama ni mwanafunzi, nilifahamu ameshamaliza Kidato cha Nne mwaka jana,” amesema Sylivesta.

Awali akijieleza mbele ya Kamati hiyo, Bundala Mashiku amesema hakujua kama mke wake alikuwa mwanafunzi na kwamba kama angekuwa anafahamu hali hiyo asingefanya uamuzi wa kumuoa kwa kuwa anafahamu sheria za nchi zinakataza ndoa za aina hiyo.