MKUU WA MKOA WA ARUSHA AFUNGUA ZOEZI LA UKAGUZI WA VYOMBO VYA MOTO

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha 

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa John Mongela  amefungua rasmi zoezi la ukaguzi wa vyombo vya moto kuelekea maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 15.11.2021 hadi tarehe 20.11.2021.

Katika ufunguzi huo uliofanyika leo  Oktoba 23, 2021 Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mbali na kupongeza Jeshi la polisi kupunguza matukio ya ajali za barabarani na ubunifu wa kwenda katika maeneo ya wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto kwa ajili ya kukagua vyombo vyao, amewapongeza wadau wa usalama barabarani hususani madereva kwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya ukaguzi wa vyombo vyao.

Aidha amesema ni muhimu Wananchi waendelee kuelimishwa kuhusiana na sheria za usalama barabarani na kukemea vitendo vya rushwa kwa Askari wachache ambao wanachafua taswira ya Jeshi la Polisi.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza maadhimisho hayo kitaifa yafanyike Mkoa wa Arusha, hivyo akatoa wito kwa wadau wa usalama barabarani kushikama na kujitoa kwa pamoja  ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa hali ya amani na utulivu.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema kama Watumiaji wa vyombo vya moto watafuata kauli mbiu ya utii wa Sheria bila shuruti watapunguza ajali nyingi za barabarani ambazo zimepelekea watu wengi kupoteza maisha, ulemavu pamoja na uharibu wa vyombo vya moto.

Awali akitoa taarifa fupi kuhusu  maadhimisho hayo Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Solomon Mwangamilo amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutoa nafasi kwa baraza la usalama barabarani kufanya tathmini ya jumla kwa mwaka mzima kuhusiana na usalama wa watumiaji wote wa vyombo vya moto, kuangalia maeneo ambayo yanapelekea ajali nyingi za barabarani na kuja na mikakati ya kupunguza ajali izo.

Amesema katika wiki hiyo watatoa elimu ikiwa ni pamoja na kukagua vyombo vyote vya moto vilivyopo mkoani Arusha, ambapo amesema wametenga maeneo tofauti kwa ajili ya zoezi hilo kwa kuzingatia ukubwa wa Jiji, ambapo alisema litafanyika katika vituo vya Polisi, viwanja vya Soweto na kwa upande wa wanaomiliki idadi kubwa ya vyombo vya moto watapeleka Wakaguzi wa magari kwenda kufanya ukaguzi katika maeneo yao baada ya kupokea maombi lengo likiwa ni kupunguza ucheleweshwaji wa utoaji huduma.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Bwana Zelote Steven pamoja na viongozi mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments