Na Dotto Kwilasa, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kuweka mikakati madhubuti na malengo yanayopimika ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza kuwa kila mkoa unapaswa kuchukua jukumu la kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kwa vitendo ili kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Amesema licha ya hatua zilizopigwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, bado kuna kazi kubwa, hususan katika mikoa ambayo imeonekana kuwa nyuma katika matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Katavi.
Akizungumza wakati wa kikao kazi na wakuu wa mikoa kuhusu utekelezaji wa mkakati huo, Dodoma Leo November 28,2026 Dkt. Nchemba alisema ni muhimu viongozi hao kuhakikisha kila mkoa unaweka mpango maalumu wa kuongeza matumizi ya nishati safi, ukiwemo mpango wa kuhamasisha shule, magereza na taasisi nyingine kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya mkakati huo hayatapimwa kwa idadi ya nyaraka na mipango inayoandaliwa, bali matokeo halisi yanayopatikana kwa wananchi, akiwataka wakuu wa mikoa kufuatilia maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa mkakati huo Mei 8, 2024.
Alisema kila mkoa unapaswa kuweka viashiria vya utekelezaji vinavyopimika, akitoa mfano wa kuanza na angalau shule 10 za bweni katika kila mkoa ili kuhakikisha zinahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, badala ya kuweka mipango isiyo na muda wala malengo mahsusi.
Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia si suala la nishati pekee, bali linahusisha afya, mazingira, uchumi na ustawi wa jamii, akibainisha kuwa matumizi ya kuni na mkaa yanaendelea kuchangia uharibifu wa misitu na madhara ya kiafya yanayotokana na moshi, pamoja na kupoteza muda ambao wanawake na watoto wangeutumia katika shughuli za uzalishaji na elimu.
Katika hatua nyingine, aliwataka wakuu wa mikoa kuunganisha mkakati huo na juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kuhakikisha kila kijiji, mtaa na kitongoji kinakuwa na kitalu cha miti, akisisitiza kuwa pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi, upandaji miti ni muhimu katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Dkt. Felchesmi Mramba, alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 6.9 wakati mkakati unaanza hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, huku makadirio yakionyesha kufikia asilimia 35 ifikapo mwisho wa mwaka 2026.
Alisema katika kipindi cha utekelezaji wa mkakati huo, majiko banifu 145,659 yamesambazwa, mitungi ya gesi ya LPG 484,410 imetolewa, huku kaya 2,515 na taasisi 31 zikiunganishwa na gesi asilia. Aidha, taasisi 2,703 zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dkt. Mramba alisema Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuimarisha uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati safi, pamoja na kupanua matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo gesi, umeme, biogas, bioethanol na majiko banifu ili kufikia lengo la kitaifa la asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.





TAFUTA HABARI
Social Plugin