Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AWAHASA WAHITIMU KUJITENGENEZEA FURSA ZA KIUCHUMI


-Amesema elimu ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na ushindani katika soko la ajira

Na. OWM (KAM) - Tabora

Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia elimu na ujuzi walioupata kujiajiri, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kubuni njia za kutatua changamoto za kijamii badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.

Amesema mabadiliko katika soko la ajira yanahitaji wahitimu kuwa wabunifu, kujiamini na kuthubutu kutekeleza mawazo yao ili kujitengenezea fursa za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Dkt. Mwigulu ametoa wito huo leo, Novemba 28, 2026, wakati akihutubia Mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo (AMUCTA), yaliyofanyika mkoani Tabora.

Amesema hali ya soko la ajira imebadilika ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo baadhi ya wahitimu walikuwa wakipata ajira hata kabla ya kukamilisha masomo yao, huku ongezeko la idadi ya wahitimu likiambatana na ushindani mkubwa wa kupata nafasi za ajira.

Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wahitimu kutokata tamaa wanapokabiliwa na changamoto za kutafuta ajira, bali watumie maarifa na ujuzi walionao kubuni fursa nyingine za kujipatia kipato.

Aidha, amewataka kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii pamoja na mahitaji ya soko la ajira.

Awali, akitoa salamu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema Serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya taifa na inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi hizo.

Amesema hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuanzisha jukumu maalumu la kuratibu mahusiano kati ya Serikali na makundi ya kijamii na kulikabidhi Ofisi ya Waziri Mkuu ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano huo.

Ameongeza kuwa taasisi za dini zimekuwa washirika muhimu wa Serikali katika kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa kupitia vikao vya mashauriano, utoaji wa elimu ya amani kwa waumini na wananchi, pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii katika sekta za elimu, afya na maji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo, Padri Profesa Juvenalis Asantemungu, amesema chuo hicho kinaendelea kuimarisha utoaji wa elimu maalumu na jumuishi kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 714 wametunukiwa tuzo mbalimbali za kitaaluma, wakiwemo wahitimu 676 wa Shahada ya Elimu ya Mahitaji Maalumu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com