Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amekutana na wananchi wa Kijiji cha Mwabomba, Kata ya Idaina, Wilaya ya Ushetu, katika kampeni ya Ongea na Kamanda, iliyolenga kusikiliza kero na changamoto za kiusalama zinazowakabili wananchi.
Mkutano huo uliofanyika leo, Oktoba 9, 2026, ulihudhuriwa na wananchi wanaokadiriwa kufikia 600, viongozi wa Jeshi la Polisi, Diwani wa Matiasi, Matias Makashi, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara, Salehe Mohamedi Mahige, pamoja na Mwenyekiti wa Maafisa Wasafirishaji, Loseliani Kilamwe.
Akizungumza katika mkutano huo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ushetu (OCD) alimweleza Kamanda Magomi hali ya usalama katika wilaya hiyo kabla ya kumkaribisha kuzungumza na wananchi.
MAGOMI AWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA ZA UHALIFU
Akizungumza na wananchi, Kamanda Magomi aliwataka kutoiogopa Jeshi la Polisi, bali kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu na matukio ya uhalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Pia, aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Niño na madhara yanayoweza kujitokeza.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza wenye silaha wasizo na vibali kuzisalimisha kwa mamlaka husika, akieleza kuwa muda wa kufanya hivyo unaelekea ukingoni mwezi Oktoba 31 mwaka huu.
Kuhusu shughuli za uchimbaji wa dhahabu, Kamanda Magomi alisisitiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu za majina ya watu wanaoingia kwenye mashimo ya migodi ili kurahisisha utambuzi na uokoaji endapo kutatokea ajali ya shimo kubomoka.
WANANCHI WATAJA CHANGAMOTO ZA USALAMA NA MADINI
Baada ya maelezo ya Kamanda Magomi, wananchi walipata fursa ya kueleza kero, maoni na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi.
Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa ni ombi la kujengewa kituo cha polisi katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Wananchi hao walisema uwepo wa kituo cha polisi utasaidia kuongeza imani ya wawekezaji wanaotaka kuanzisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, lakini wanakabiliwa na hofu kuhusu usalama wa mali zao.
Pia, walihoji mikakati iliyowekwa na Serikali kukabiliana na madhara ya kemikali zenye sumu zinazotumika katika uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu, hususan iwapo mvua kubwa zitasababisha kemikali hizo kusambaa na kuathiri wananchi na mazingira.
Hoja nyingine iliyotolewa ilihusu umri unaoruhusiwa kwa watoto kushiriki au kuingia katika maeneo ya machimbo ya madini, huku wananchi wakitaka ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa kulinda watoto dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza migodini.
Aidha, wananchi walipendekeza kuruhusiwa kukata kuni au mkaa katika maeneo ya Hifadhi ya Moyowosi-Kigosi ili kuwa na akiba ya nishati itakayoweza kuwasaidia iwapo mvua kubwa za El Niño zitasababisha changamoto za upatikanaji wa nishati.
Kampeni ya Ongea na Kamanda ni fursa ya wananchi kuwasilisha changamoto zao za kiusalama moja kwa moja kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, huku ikihamasisha ushirikiano kati ya polisi na jamii katika kuzuia uhalifu na kuimarisha usalama.











Social Plugin