Na Marco Maduhu, Elizabeth Cosmas, SHINYANGA
Wananchi wa Kijiji cha Nyida wilayani Shinyanga, wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, kwa kuendelea kuwasemea Bungeni, kuhusu ukamilishaji wa Skimu ya Umwagiliaji.
TAZAMA VIDEO👇👇
Wamebainisha hayo leo Septemba 26, 2026, katika mkutano wa hadhara wa Mbunge Azza, wa kuwashukuru wananchi pamoja na kusikiliza kero zao na kuzitolea majibu.
Katibu wa Skimu ya umwagiliaji Masele Nyanza, amesema kupitia vyombo vya habari, wameona na kusikia namna ambavyo Mbunge huyo amekuwa akiwasemea Bungeni kuhusu mradi huo wa Skimu ya Umwagiliaji.
“Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi chako cha miezi nane, tumekuwa tukipokea ugeni wa mara kwa mara kitaifa wa kukagua ujenzi wa bwawa, ambao hadi sasa umefikia asilimia 93. Hongera sana,” amesema Nyanza.
Naye Malija Luhende, amesema licha ya kero yake kuwa tayari Mbunge ameshaisemea, lakini amekumbushia kuhusu mrefeji mpya, ambao tayari imeshafanyiwa michoro kwa ajili ya Heka nyingine 379.
“Tunakuomba Mbunge wetu uendelee kutusemea zaidi juu ya mradi huu wa skimu ya umwagiliaji, ili ukamilike na kuanza kuutumia kwa shughuli za kilimo, sababu skimu hii ni ya mfano kwa Kanda ya Ziwa,” amesema Luhende.
Kwa upande wake Mbunge Azza, amesema mradi huo wa Skimu ya Umwagiliaji tayari ameshausemea Bungeni, na kwamba Waziri husika ameahidi kufanya ziara katika skimu hiyo kwa kuutembelea.
Aidha, katika mkutano huo, amezungumzia pia suala la upatikanaji wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, pamoja na usambazaji wa umeme wa REA katika ngazi ya vitongoji.
Katika mikutano yake ya hadhara aliyofanya leo katika Vijiji vya Puni na Nyida, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El Niño ili kuepuka madhara.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, yupo katika ziara yake ya kijiji kwa kijiji jimboni kwake.
TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Diwani wa Nyida Seleman Seregeti akizungumza.
Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad akitembelea mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Nyida.



















Social Plugin