
Na Bora Mustafa, Dar es Salaam.
Taasisi ya Media Brains, kwa kushirikiana na Taasisi ya Kijerumani ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS), imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa kuchambua, kutambua na kuhakiki taarifa zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii kabla ya kuzifikisha kwa umma.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu, kuanzia Septemba 23 hadi 25, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Media Brains, Jesse Kwayu, amesema kuongezeka kwa taarifa za uongo katika jamii kunahitaji waandishi wa habari kuwa na ujuzi zaidi wa kuchambua taarifa na kutumia mbinu sahihi za uthibitishaji kabla ya kuzichapisha.
Kwayu amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuwajengea waandishi uwezo wa kukabiliana na changamoto za taarifa za uongo zinazozagaa katika mitandao ya kijamii, huku akibainisha kuwa moja ya maeneo yaliyosisitizwa ni namna ya kukabiliana na kuenea kwa taarifa za uongo katika jamii.
“Tumekuwa na mfululizo wa mafunzo ambao unafanyika hapa Tanzania, ni wazi kwamba waandishi wa habari wanatakiwa kuwa makini katika kuchambua na kuhakiki taarifa kabla ya kuzifikisha kwa umma, kutokana na kasi ya usambazaji wa taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii,” amesema Kwayu.
Kwa upande wa Ofisa Uendeshaji Mkuu wa Media Brains, Absalom Kibanda, amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa waandishi kuhusu changamoto zinazotokana na upotoshaji mkubwa wa taarifa katika mitandao ya kijamii, hali ambayo amesema si changamoto inayokabili Tanzania pekee bali imekuwa suala linaloonekana katika sehemu mbalimbali duniani.
Kibanda amesema mabadiliko ya teknolojia yameongeza kasi ya usambazaji wa taarifa, ikiwemo misinformation, disinformation na malinformation, hivyo waandishi wa habari wanapaswa kuwa na uwezo wa kuchunguza ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji.
“Tunatoa mafunzo ili kufanya kile ambacho kinafanya tupate kila habari, iwe ni video au habari tunazopokea kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, WhatsApp na YouTube, kujua ukweli wake kama ni habari ya kweli kabla haijawafikia wanajamii au wadau wa habari,” amesema Kibanda.
Aidha, amesema kuenea kwa taarifa za uongo na upotoshaji kumechangia kupungua kwa imani ya wananchi katika habari, jambo linalowataka waandishi wa habari kuongeza umakini katika mchakato mzima wa ukusanyaji, uchambuzi, uhakiki na uchapishaji wa taarifa.
Hata hivyo, Kibanda amesema Media Brains kwa kushirikiana na KAS imeendelea kutoa mafunzo ya kidijitali katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwapa wanahabari uelewa na uzoefu wa kutambua taarifa za kweli na zile zinazoweza kuwa zimetengenezwa kwa makusudi au kusambazwa kwa malengo ya kupotosha.
Pia, amesema mafunzo hayo yanawasaidia wanahabari kuendelea kujifunza na kutumia zana mbalimbali za teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili bandia, katika mchakato wa kuchunguza na kuhakiki taarifa.



Social Plugin