Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

STANDARD CHARTERED FOUNDATION YATOA TZS MILIONI 21.4 KUWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI KUPITIA PROGRAMU YA MABINTI YA CCBRT







Standard Chartered Foundation, kupitia Standard Chartered Tanzania, imetoa mchango wa TZS 21,456,431.52 kwa ajili ya kuunga mkono Programu ya Mabinti ya CCBRT, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Benki ya kuendelea kukuza ujumuishaji wa kiuchumi na kuongeza fursa kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu nchini Tanzania.

Mchango huo utagharamia programu ya wiki sita itakayowanufaisha wanawake 40 kupitia mafunzo ya stadi za kazi, usimamizi wa biashara na elimu ya fedha, pamoja na ununuzi wa mashine za kushona zitakazowawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za kujiongezea kipato.

Kupitia ufadhili huo, washiriki watapatiwa mafunzo ya ushonaji wa bidhaa za crochet, urembaji wa nguo (embroidery), usimamizi wa biashara na elimu ya fedha. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wanawake ujuzi wa vitendo na maarifa ya ujasiriamali yatakayowawezesha kujitegemea kiuchumi. Aidha, mashine za kushona zitakazonunuliwa kupitia mchango huo zitawasaidia kuongeza uzalishaji na kipato baada ya kuhitimu mafunzo.

Programu ya Mabinti inayotekelezwa na CCBRT inawalenga wanawake walio katika mazingira magumu, wakiwemo wanawake wenye ulemavu, manusura wa fistula ya uzazi, wasichana walioacha shule na wanawake wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii. Kupitia mafunzo ya ujuzi na usaidizi wa ujasiriamali, programu hiyo inawawezesha wanawake kujitegemea kifedha na kuboresha maisha yao.

Ushirikiano huu unaendelea kudhihirisha dhamira ya Standard Chartered ya kuwekeza katika maendeleo ya jamii inazohudumia. Mapema mwaka huu, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, wafanyakazi wa Standard Chartered Tanzania walitembelea Kituo cha Mabinti na kukabidhi mashine 12 za kushona pamoja na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanufaika wa programu hiyo. Hatua hiyo ilionesha dhamira ya Benki ya kuwawezesha wanawake kupitia msaada wa vitendo na kuwajengea uwezo.

Mchango huu pia umetolewa katika mwaka ambao Standard Chartered inaadhimisha miaka 20 ya Mpango wa Kujitolea wa Wafanyakazi, unaotambua mchango wa wafanyakazi wake ambao kwa kipindi cha miongo miwili wamekuwa wakitumia muda, ujuzi na uzoefu wao kuleta mabadiliko chanya katika jamii duniani.

Akizungumza kuhusu mchango huo, Afisa Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Coverage wa Standard Chartered Tanzania, Geofrey Mchangila, alisema:

"Tunajivunia kuendeleza ushirikiano wetu na CCBRT katika kuunga mkono Programu ya Mabinti ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha wanawake. Hii ni mara ya pili kushirikiana na CCBRT. Mapema mwaka huu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, timu yetu ilitembelea kituo hicho, ambapo tulikabidhi mashine 12 za kushona na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanawake wanaoshiriki katika programu hiyo.

Leo tunaimarisha zaidi dhamira yetu kwa kutoa TZS milioni 21.4 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya stadi za kazi, usimamizi wa biashara na fedha kwa wanawake 40, pamoja na ununuzi wa mashine zaidi za kushona. Tunaamini kuwa programu kama hii zinawapa wanawake ujuzi, maarifa na rasilimali muhimu za kujenga maisha ya kujitegemea na mustakabali wenye fursa zaidi."

Afisa Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Coverage wa Standard Chartered Tanzania, Geofrey Mchangila akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la CCBRT Brenda Msangi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi (TZS) 21,456,431.52 kwa ajili ya kuunga mkono Programu ya Mabinti ya CCBRT, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Benki ya kuendelea kukuza ujumuishaji wa kiuchumi na kuongeza fursa kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu nchini Tanzania.


Mchango huo utagharamia programu ya wiki sita itakayowanufaisha wanawake 40 kupitia mafunzo ya stadi za kazi, usimamizi wa biashara na elimu ya fedha, pamoja na ununuzi wa mashine za kushona zitakazowawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za kujiongezea kipato.

Afisa Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Coverage wa Standard Chartered Tanzania, Geofrey Mchangila akioneshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la CCBRT Brenda Msangi baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na baadhi ya Wanawake waliopo kwenye taasisi hiyo.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com