Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF.MANAMBA:NGUVU KAZI YENYE UJUZI NDIO UFUNGUO WA KUKUZA UCHUMI WA TAIFA



MKUU wa Kampasi ya Dodoma wa Chuo cha Uhasibu Arusha,Prof. Epaphra Manamba,amesema wanaendelea kuandaa wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji, usimamizi na biashara ya mazao, hatua itakayochangia kuongeza tija, ushindani na thamani ya sekta ya kilimo nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt.John Malecela Nzunguni jijini Dodoma, Mkuu wa Kampasi ya Dodoma wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Prof.Epaphra Manamba, akimwakilisha Mkuu wa Chuo, Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema IAA imeamua kushiriki maonesho hayo ili kuwa karibu na wakulima, kutoa elimu na kuonesha mchango wa taaluma katika kuimarisha uzalishaji wa kilimo nchini.

Amesema sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwa kuwa inategemewa na takribani asilimia 65 ya nguvu kazi ya Taifa, lakini bado mchango wake katika Pato la Taifa ni takribani asilimia 26 pekee, hali inayoonesha kuwa kuna nafasi kubwa ya kuongeza tija kupitia matumizi ya maarifa, teknolojia na usimamizi bora wa biashara.

"Kilimo kinahitaji nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na maarifa ya kisasa. Ndiyo maana Chuo cha Uhasibu Arusha kinaendelea kutoa programu mbalimbali za biashara, uchumi, fedha na teknolojia ili kuwajengea uwezo wataalamu watakaosaidia kuifanya sekta ya kilimo iwe yenye ushindani na yenye mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa," amesema Prof.Manamba.

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto za mitaji zinazowakabili wakulima wengi pamoja na utegemezi wa zana duni za kilimo, bado kuna fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji endapo wakulima wataunganishwa na taasisi za kifedha pamoja na huduma za kitaalamu zitakazowezesha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika teknolojia za kisasa.

Prof.Manamba amesema IAA imejikita pia katika kufundisha teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), ambapo wanafunzi wa chuo hicho tayari wamebuni mifumo inayotumia AI kuboresha uzalishaji wa mazao kama vitunguu kwa lengo la kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kuifanya kilimo kuwa biashara yenye faida zaidi.

"Hatutaki kuona kilimo kinabaki kwa ajili ya kujikimu pekee. Tunataka wakulima walime kwa mtazamo wa biashara, waongeze thamani ya mazao yao na kuongeza kipato cha familia zao pamoja na kuchangia zaidi katika uchumi wa Taifa," amsisitiza.

Akizungumzia kaulimbiu ya Nanenane ya mwaka huu isemayo "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa 2050," Prof.Epaphra Manamba amesema dira hiyo inalenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa inayoweza kuleta mapinduzi katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan kilimo.

Amebainisha kuwa taasisi za elimu zina jukumu la kuhakikisha zinatoa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kuifanya Tanzania kufikia malengo ya maendeleo ya Dira ya Taifa 2050.

Amesema kupitia ushiriki wa Maonesho ya Nanenane, Chuo cha Uhasibu Arusha kinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu programu zake mbalimbali na namna zinavyoweza kuwaandaa vijana kuwa wataalamu watakaochangia maendeleo ya kilimo, biashara na uchumi wa kidijitali nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com