Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AZINDUA TUME YA UCHUNGUZI WA GHASIA NA UKIUKWAJI WA SHERIA ATAKA WATANZANIA KUIPA USHIRIKIANO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka Watanzania kuipa ushirikiano wa kutosha na kutoiingilia wala kuisumbua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wakati ikitekeleza majukumu yake mazito.

Akizungumza leo Agosti 7, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi tume hiyo ambayo imepewa muda wa miezi mitano kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti, Rais Samia alieleza kuwa jukumu hilo si jepesi na linahitaji umakini wa hali ya juu, huku akiwashukuru Makamishna wa tume hiyo kwa kulipokea jambo hilo na kuwatakia majukumu mema.

“Nawasihi sana Watanzania tuiunge mkono tume hii na tusiisumbue katika kutekeleza majukumu yake,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alifafanua kuwa uamuzi wa kuunda tume hiyo chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, umetokana na mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, ambayo aliyapokea Aprili 23, mwaka huu.
Alisema kuwa tume hiyo ilipendekeza kufanyika uchunguzi wa kina ili kubaini waliochochea, waliohusika, na waliofadhili matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi ili hatua za uwajibikaji zichukuliwe kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa serikali imeamua pia kuwashirikisha majaji kutoka Uganda na Namibia ili kupata mtazamo mpana na kuongeza uwazi katika utekelezaji wa kazi hiyo, huku muda huo wa miezi mitano ukiweza kuongezwa endapo kutakuwa na sababu za msingi .
Akitoa wasifu wa wajumbe wa tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka alisema Mwenyekiti wa tume ni Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaaban Ali Lila ambaye pia aliwahi kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Mtwara na Msajili wa Mahakama Kuu katika kanda za Mbeya, Dar es Salaam na Arusha.

Alimtaja Mjumbe kutoka Namibia ni Jaji Petrus Damaseb ambaye ni Naibu Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Namibia. Pia, ni Jaji wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo. Amewahi kuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namibia, Jaji wa Rufani wa Mahakama ya Rufani ya Lesotho na Kaimu Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Botswana.

Mjumbe kutoka Uganda ni Jaji Barishaki Cheborion ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda na Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki ngazi ya rufaa. Amehudumu katika tume mbalimbali za uchunguzi nchini Uganda zikiwamo za ukiukwaji wa haki za binadamu, uchunguzi wa tukio la kuchomwa moto Makaburi ya Kasubi na tuhuma za rushwa mjini Mbarara.

Wajumbe wengine ni Jaji mstaafu Gadi Mjema aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mwenyekiti wa Bodi ya Rufani za Kodi (TRAT).

Yumo Jaji mstaafu Awadh Mohamed Bawazir aliyewahi kuwa Mchunguzi Mkuu na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke.

Pia, Jaji mstaafu Aishieli Nelson Sumari aliyewahi kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda za Moshi na Mwanza na Mkurugenzi Msaidizi wa Makosa ya Udanganyifu na Rushwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dk Kusiluka alisema tume hiyo itasaidiwa na Sekretarieti ya watu sita inayoongozwa na Paul Kadushi, huku maandalizi yote ya kuanza kazi yakiwa yamekamilika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com