
Katika kuleta tija kwenye mpango huo mpana wa maendeleo ya mijini na usafiri jumuishi, Rais Samia alianika mpango mpya wa kupanua Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka katikati ya jiji hadi kufika katika wilaya za Mkuranga, Kisarawe, na Bagamoyo mkoani Pwani.
Alieleza hayo Dar es Salaam wakati akizindua miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka ya Awamu ya Pili (BRT II) katika barabara za Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa.
“Tunakwenda kwenye kupanga Jiji la Dar es Salaam, hiyo ndio kazi ambayo iko mbele yetu. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wataishi mijini, hivyo ukuaji wa miji yetu lazima uongozwe na mipango inayotazama mahitaji ya muda mrefu, kwa hiyo tutatoka sasa kwenye nyumba zile lakini nadhani tutaweza kwenda nyumba za kunyanyuka ili watu wengi zaidi waingie wakae katika nyumba hizi,” alifafanua.
Akifafanua kuhusu BRT alisema katika awamu ya pili ambayo ni barabara inayotoka katikati ya mji hadi Mbagala Rangi Tatu, barabara hiyo baadaye itafika hadi Mkuranga huku kwa awamu ya tatu kutoka katikati ya mji hadi Gongo la Mboto itafika hadi Kisarawe na awamu ya nne inayotoka katikati ya mji hadi Bunju, itafika hadi Bagamoyo.
“Sasa mpango wetu wa baadaye ni kutanua, kuongeza njia hii tunapozungumzia njia hii ya Mbagala Rangitatu lengo letu ni kupeleka mpaka Mkuranga, sasa wataalamu wanafanyia kazi. Ile ya Bunju nayo tukifika Bunju tuna nia ya kuipeleka mpaka Bagamoyo kwa sababu Bagamoyo inakwenda kuwa Mji wa eneo huru la biashara na eneo la uchumi, kuna bandari kubwa kule, kuna eneo huru la uchumi mkubwa,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wa Bagamoyo alisema inajengwa Reli ya Kisasa (SGR) kuunganisha Bandari ya Bagamoyo kwenda Kwala na eneo la huru la uchumi kwa ajili ya mizigo kuwa barabara itakayounganishwa kutoka Bunju hadi Bagamoyo itasaidia wafanyakazi, wenye bidhaa, wafanyabiashara kusafiri haraka kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
Aliwataka Watanzania hususani vijana, kulinda miundombinu inayojengwa na serikali kwa gharama kubwa, akisisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu hiyo unarudisha nyuma maendeleo ya taifa na kuwaongezea wananchi gharama zisizo za lazima.
“Hatuwezi kutumia miaka mingi kutafuta fedha kujenga miundombinu na kuanza kutoa huduma, halafu tukakubali juhudi hizo ziteketezwe ndani ya muda mfupi. Hii haikubaliki,” alisema.
Aliongeza kuwa uharibifu wa miundombinu unaibebesha serikali gharama kubwa za kurekebisha na fedha hizo zingetumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo na kwamba anayefanya hivyo anachelewesha maendeleo ya taifa, analivuta nyuma taifa, ni mhujumu uchumi na ni adui wa taifa.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alibainisha kuwa mradi huo unarahisisha maisha ya wananchi na kulinda mazingira kupitia matumizi ya gesi asilia, kauli iliyoungwa mkono na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Sidi Ould Tah, aliyetangaza utayari wa benki hiyo kuendelea kuisaidia Tanzania. Sambamba na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2025 inayoelekeza kuboresha miundombinu ya usafiri, mradi huo umeanza kuleta mafanikio makubwa kwa kupunguza muda wa safari kutoka zaidi ya saa moja hadi dakika thelathini na kupunguza msongamano jijini.
Social Plugin