Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AZZA: BARABARA YA NJIA PANDA LUHUMBO–DIDIA KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI, LUHUMBO SEKONDARI IMEPOKEA MIL. 113 KWA MADARASA

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Didia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 7, 2026, ambapo ametoa mrejesho wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kueleza kuwa barabara ya Njia Panda ya Luhumbo–Didia yenye urefu wa kilomita 4.5 inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, pamoja na kuwasikiliza wananchi na kujibu kero mbalimbali. Picha na Kadama Malunde
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Didia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 7, 2026.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Didia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Agosti 7, 2026. Picha na Kadama Malunde

Na Marco Maduhu, Shinyanga

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, amesema barabara ya kutoka Njia Panda ya Luhumbo hadi Didia yenye urefu wa kilomita 4.5 inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, hatua itakayorahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo.

Azza ameyasema hayo leo Agosti 7, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Didia katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero zao na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali za maendeleo.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa miongoni mwa maombi makubwa yaliyotolewa na wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi, na kwamba tayari suala hilo limewasilishwa bungeni huku Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga ukiwa umekamilisha tathmini na kuwasilisha taarifa TAMISEMI kwa hatua zaidi.
"Changamoto ya barabara ya kutoka Njia Panda ya Luhumbo hadi Didia Center inaelekea kupata ufumbuzi kwa kujengwa kwa kiwango cha lami," amesema Azza.

Akizungumzia maendeleo mengine yanayotekelezwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya CCM, Azza amesema ndani ya kipindi kifupi baada ya kuanza kutekelezwa kwa ilani hiyo, fedha mbalimbali zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika eneo hilo.

Amesema Shule ya Sekondari Luhumbo imepokea shilingi milioni 113 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, huku Shule ya Msingi Didia ikipokea shilingi milioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne pamoja na ununuzi wa madawati.

Aidha, amesema majengo ya zamani ya Shule ya Msingi Didia yamechakaa kiasi kwamba yanahitaji kujengwa upya badala ya kufanyiwa ukarabati.

"Shule hii ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa. Serikali imesikia kilio cha wananchi na tayari fedha zimepatikana. Si muda mrefu tutaanza kuona shule yetu ikiwa katika mazingira bora zaidi," amesema.

Katika sekta nyingine, Azza amesema Serikali imetoa shilingi milioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Kijiji cha Didia, pamoja na shilingi milioni 438 kwa ajili ya ujenzi wa mita 300 za mitaro katika Mji Mdogo wa Didia.

Pia amesema shilingi milioni 69 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani na makalavati, huku shilingi milioni 16 zikielekezwa kujenga matundu 23 ya vyoo katika Shule ya Msingi Didia.
Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, amesema vikundi vitatu vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Mji Mdogo wa Didia vimepokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 56.9.

Azza pia amesema ameendelea kuishawishi Serikali kujenga Kituo cha Afya Didia ili kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi, akieleza kuwa ombi hilo limewasilishwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Katika mkutano huo, wananchi wamewasilisha kero mbalimbali zikiwemo ukosefu wa stendi ya mabasi, upatikanaji wa huduma ya umeme katika baadhi ya vitongoji na changamoto nyingine za miundombinu, huku Mbunge huyo akiahidi kuendelea kuzifuatilia kwa kushirikiana na Serikali hadi zipatiwe ufumbuzi.

TAZAMA VIDEO👇👇




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com