Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIMARISHA ELIMU KWA MAHITAJI YA UCHUMI WA KIDIJITALI


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SERIKALI itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya kitaaluma ya walimu, wakufunzi na wahadhiri kupitia mafunzo endelevu, tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha mfumo wa elimu unazalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kidijitali.

Ameyasema hayo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafadh Ameir, Agosti 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua hafla ya Inclusive Mwalimu Gala 2026, iliyowakutanisha walimu, wahadhiri, watafiti, wabunifu na wadau wa sekta mbalimbali kujadili nafasi ya elimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema kaulimbiu ya hafla hiyo, “The Contribution of Women Professionals to the Implementation of Tanzania Development Vision 2050,” inaonesha umuhimu wa wanawake wanataaluma katika kuendeleza utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia kama msingi wa maendeleo ya taifa.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kupitia maboresho ya sera na sheria, ujenzi wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa walimu, wakufunzi, wahadhiri, watafiti na wadau wa sekta binafsi kuendelea kushirikiana katika kuandaa kizazi chenye maadili, maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa, akisisitiza kuwa elimu inapaswa kuwa kitovu cha kuzalisha suluhisho za maendeleo na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema Mwalimu Inclusive Gala 2026 imekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha walimu wa ngazi zote na wazazi kwa lengo la kubadilishana mawazo, kutoa taarifa na kupokea maoni yatakayochangia maendeleo ya sekta ya elimu, sayansi na teknolojia nchini.

Amesema kwa upande wa COSTECH, mwaka huu taasisi hiyo pia inaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, hivyo jukwaa hilo limekuwa fursa ya kusikiliza maoni ya wadau pamoja na kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.

Ameongeza kuwa walimu wana jukumu kubwa la kuwaandaa wanafunzi ambao ndiyo wabunifu wa kesho, hivyo wanapaswa kuwafahamisha kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya sayansi na teknolojia, ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Utafiti unaoratibiwa na COSTECH.

"Walimu ndiyo wanaowaandaa wabunifu wa kesho. Kupitia mfumo huu wataweza kupata taarifa mbalimbali na kuwaongoza wanafunzi wao kutumia fursa za utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia," amesema.

Aidha, Dkt. Nungu amewahimiza walimu na wadau wengine kushiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu itakayofanyika jijini Tanga kuanzia Agosti 15 hadi 24, akisema maonesho hayo yatatoa nafasi ya kuona bunifu mbalimbali, tafiti na teknolojia zinazofanywa nchini.

Amesema majukwaa kama Mwalimu Inclusive Gala yanapaswa kuendelea kutumiwa kama sehemu ya kupata mrejesho kutoka kwa wadau kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa, sambamba na kutoa taarifa kuhusu shughuli na fursa zinazopatikana katika sekta ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

"Natoa wito kwa walimu na wadau wote walioshiriki hapa kuhakikisha wanashiriki pia maonesho ya Tanga, kwani huko watapata nafasi ya kujionea bunifu mbalimbali, tafiti zinazoendelea na fursa nyingi zaidi zinazotolewa na COSTECH". Amesema

Nae mwandaaji wa jukwaa hilo, Mbunge Mwakilishi wa Vyuo Vikuu, Mhe. Aisha Feruzi amesema Inclusive Mwalimu Gala 2026 ni jukwaa pana la kujadili mustakabali na nafasi ya elimu, ubunifu na teknolojia katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kwamba linajumuisha walimu, wahadhiri, watafiti, vijana wabunifu wanawake na wadau wa sekta binafsi.

Amesema kuwa matokeo yanayotarajiwa kupitia kongamano hilo ni kuimarika kwa tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan akili unde (Artificial Intelligence) na ushirikiano kati ya elimu na viwanda.

Ameongeza kuwa vyuo vikuu na sekta binafsi vitaunganishwa ili kuzalisha suluhisho, bidhaa na huduma zinazochochea ukuaji wa uchumi shindani na endelevu. -

Aidha, ameeleza kuwa kupitia mijadala ya kitaaluma, washiriki wanatarajiwa kujifunza kutokana na maendeleo yaliyopatikana katika sayansi na teknolojia, uchumi wa kidijitali, tafiti, elimu na ubunifu wa biashara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com