Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA, MAREKANI ZAJADILIANA USHIRIKIANO



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, walifanya mazungumzo rasmi na ujumbe maalum wa wajumbe 11 kutoka Baraza la Wawakilishi la Marekani (Congress), ulioongozwa na Ronny Jackson, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Huduma za Kijeshi, Ulinzi na Usalama ya Baraza hilo, katika Makao Makuu ya zamani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Ngome Upanga, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Tanzania ilitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa kuondolewa kwa vikwazo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masharti na taratibu ngumu za utoaji wa visa kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nchini Marekani, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibinadamu na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.


Kwa upande wao, ujumbe huo wa Marekani uliipongeza Tanzania kwa nafasi yake kubwa na mchango thabiti katika kudumisha amani, usalama wa kikanda, juhudi za kupambana na ugaidi, na ushiriki wake mkubwa katika operesheni za kulinda amani barani Afrika. Pande zote mbili ziliafikia makubaliano ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maeneo ya maslahi ya pamoja huku zikiweka mikakati ya kuendeleza majadiliano ya kina kuhusu masuala yote yaliyowasilishwa na upande wa Tanzania katika vikao vijavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com