-Atoa siku 14 Kituo cha Kitaifa cha Oparesheni kianze kufanya kazi
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa siku 14 kwa wizara na taasisi zinazohusika na Kituo cha Kitaifa cha pamoja cha Oparesheni zipeleke wawakilishi ili kianze kufanya kazi mara moja.
"Wizara na taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa majukumu katika Kituo cha Kitaifa cha pamoja cha Oparesheni zipeleke wawakilishi wote wanaohitajika ndani ya siku 14 kuanzia leo. Kituo hiki kianze kazi mara moja ili kuleta tija inayokusudiwa," amesema Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu ametoa wito huo leo (Ijumaa, Julai 31, 2026) wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya makabidhiano na uzinduzi wa boti mbili za doria aina ya PB Sailfish 02 na PB Sailfish 03 iliyofanyika bandarini, jijini Dar es Salaam. Boti hizo zimenunuliwa kwa thamani ya dola za Marekani milioni 1.6.
Amezitaka Wizara za Muungano zinazohusika na suala hilo zishirikiane ili kuziba chochoro zote ambazo zingetumiwa na wahalifu katika eneo hili tunalolilenga na hasa katika mipaka ya mwambao wa bahari.
Ili kuhakikisha boti hizo zinafanya kazi kama inavyotarajiwa, Waziri Mkuu ameziagiza wizara na taasisi zote za umma zinazohusika katika matumizi ya boti hizi za doria zitenge fedha kwa ajili ya kazi za boti hizi.
"Ninasisitiza suala la kutenga bajeti ili kazi za doria zisikwamishwe na ukosefu wa bajeti. Nimekuwa nikikutana na kesi kama hizo mikoani ambapo Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alinunua ambulance za kisasa na nyingine zina ICU lakini zinashindwa kuhudumia wagonjwa kwa wakati kwa kukosa mafuta. Hili linakinzana na dhamira njema ya Mheshimiwa Rais ya kutaka kuokoa maisha ya Watanzania pindi wanahitaji huduma hizo," amefafanua.
Akielezea umuhimu wa boti hizo za doria, Waziri Mkuu amesema makabidhiano ya boti hizo ni tukio muhimu kiuchumi kwa sababu zinaenda kulinda mazao yatokanayo na uchumi wa bluu. Amesema uhitaji wa boti hizo umekuwa ni kilio cha muda mrefu tangu yeye akiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Amesema upatikanaji wa boti hizo mbili, utaimarisha ulinzi hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania ni lango la nchi nyingi zikiwemo za Afrika Mashariki na za SADC lakini usalama utakaokuwepo unahusu Tanzania na wananchi wa hizo nchi jirani.
"Wananchi kutoka nchi hizo watakuwa na uhakika wa usalama watakapotumia lango la bandari ya Dar es Salaam," amesisitiza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi alisema ununuzi wa boti mbili za doria aina ya PB Sailfish 02 na PB Sailfish 03 ulifanyika baada ya kukamilika kwa taratibu zote za manunuzi ambapo mkataba wa ununuzi ulisainiwa Julai 29, 2025 kati ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini na Kampuni ya Yamaha Motors Co. Ltd.
“Ujenzi wa boti hizo ulifanyika nchini Japan kwa kuzingatia vipimo na viwango vya kimataifa vilivyokubaliwa na wataalamu wa Serikali. Hadi kukamilika kwake, ujumbe wa wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, TASAC, UNDP na Chuo cha Mipango ulifanya ziara za ukaguzi ili kujiridhisha na ubora wa kazi iliyotekelezwa,” alisema.
Naye, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mikami Yoichi alisema kijiografia Tanzania na Japan ziko mbali lakini zinaunganishwa na bahari za Hindi na Pasifiki na kwamba uwepo wa usalama kwenye mipaka ya baharini, kuwahakikishia wananchi wake usalama wa maisha yao.
Alisema ana imani kwamba Serikali ya Tanzania itahakikisha boti hizo zinatumika kwa miaka mingi kwa faida ya vizazi vijavyo.











Social Plugin