NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wametakiwa kutumia maarifa, ubunifu na teknolojia kuleta mabadiliko chanya katika jamii, huku wakihimizwa kuwa tayari kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa inayohitaji uadilifu, uwezo wa kuendana na mabadiliko pamoja na ujasiri wa kutatua matatizo halisi ya kijamii.
Wito huo umetolewa Mei 25, 2026 na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi Mwanaidi Maajar wakati wa Mahafali ya 56 ya chuo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kutunuku wahitimu digrii za uzamivu, umahiri, stashahada za uzamili, digrii za awali, stashahada na astashahada.
Akizungumza katika mahafali hayo, Balozi Maajar amesema dunia ya sasa imejengwa katika misingi ya maarifa, ubunifu na matumizi ya teknolojia, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia elimu waliyoipata si kwa manufaa yao binafsi pekee, bali kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Amesema maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) yameifanya dunia kuwa ya ushindani mkubwa, ambapo uwezo wa kutumia maarifa kwa vitendo, kufanya ubunifu na kuhimili mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ni miongoni mwa sifa muhimu zinazohitajika katika soko la ajira na ujenzi wa uchumi wa kisasa.
“Mafanikio yenu hayatapimwa kwa vyeti mlivyopata pekee, bali kwa mchango mtakaoutoa katika kuboresha maisha ya watu na kujenga taifa letu,” amesema Maajar.
Ameongeza kuwa chuo kimewapatia wahitimu maarifa, maadili, uwezo wa kufikiri kwa ubunifu na msingi wa kutoa huduma bora kwa jamii, huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho kwa kujenga taasisi imara, kuendeleza uongozi wenye maadili na kushiriki katika maendeleo endelevu ya Tanzania na dunia kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Balozi Maajar ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ya juu kupitia ajira za watumishi wapya, akibainisha kuwa katika mwaka wa masomo 2025/2026 jumla ya watumishi wapya 345 walijiunga na chuo hicho, wakiwemo watumishi wa taaluma 193 na watumishi wa kada za uendeshaji 172, hatua iliyoongeza nguvu kazi ya chuo.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. William Anangisye amesema chuo kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu kwa kufanya mapitio ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia.
Amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026 jumla ya mitaala 285 ya shahada za awali na uzamili imepitiwa kwa kuzingatia maoni ya wadau, ambapo mitaala 246 imewasilishwa kwa Tanzania Commission for Universities kwa ajili ya ithibati na kati yake mitaala 146 tayari imeidhinishwa.
Aidha, amesema mitaala 99 imeandaliwa kutolewa kwa mfumo wa mseto kupitia Moodle LMS, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa elimu na kuendana na maendeleo ya kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji.
Katika eneo la utafiti na ubunifu, Prof. Anangisye amesema kwa mujibu wa AD Scientific Index 2026, chuo hicho kina watafiti 235 kati ya watafiti 1,000 bora nchini Tanzania, sawa na asilimia 23.5 ya uwakilishi katika taasisi 50, jambo linalodhihirisha nafasi yake katika uzalishaji wa maarifa na tafiti.
Ameongeza kuwa watafiti na wavumbuzi wa chuo hicho wamefanikiwa kusajili hati miliki sita katika Business Registrations and Licensing Agency katika mwaka wa masomo 2025/2026, huku baadhi ya timu za ubunifu zikijumuisha wanafunzi, hatua inayochochea ukuzaji wa tafiti zenye matokeo ya moja kwa moja kwa jamii.
Prof. Anangisye pia amesema chuo kinaendelea kupanua ushirikiano wa kimataifa kupitia ziara za kitaaluma na taasisi mbalimbali, ikiwemo ushirikiano na taasisi za elimu nchini China pamoja na mashirika ya kimataifa katika kuendeleza programu za taaluma za sayansi na tiba.
Mbali na hilo, amesema kupitia Mradi wa HEET, chuo kinaendelea na ujenzi wa majengo mapya 21 pamoja na ukarabati wa majengo matatu, hatua inayotarajiwa kuongeza nafasi za wanafunzi 4,812, huku majengo ya IMS Zanzibar, CoICT Kijitonyama na SoAF Kunduchi tayari yakikamilika na kukabidhiwa kwa matumizi.














Social Plugin