Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA ASILIMIA 60 YA WAGONJWA WA MOYO JKCI WANATOKA KANDA YA KASKAZINI







Na Oscar Assenga, Tanga

ZAIDI ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) wanatoka katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, hali inayoendelea kuchochea ujenzi wa Taasisi kubwa ya Moyo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Hospital ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akizungumza jijini Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Burian wakati wa mkutano wake na wana habari kuelezea harambee ya kuchangia ujenzi wa Taasisi Kubwa ya Moyo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC utakaofanyika Mei 30 mwaka huu katika Ukumbi wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Jijini Tanga

Alisema serikali pamoja na wadau wa maendeleo wameona umuhimu wa kuimarisha huduma za moyo Kanda ya Kaskazini kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa kutoka eneo hilo wanaohitaji matibabu ya kibingwa.


Alisema mradi huo utakaojengwa KCMC utakuwa na uwezo wa kutoa huduma za kisasa zinazolingana na zile zinazotolewa JKCI, na unatarajiwa kuhudumia wakazi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

“Mkoa wa Tanga utaungana na uongozi wa KCMC kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa mafanikio,” alisema Burian, akisisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha sekta ya afya nchini chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Burian aliongeza kuwa tayari zaidi ya Shilingi bilioni 22 zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, huku Shilingi bilioni 3 zikihitajika kukamilisha ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Kwa mujibu wa taarifa za mradi, ujenzi tayari umeanza na umefikia asilimia 40 ya utekelezaji, huku gharama ya jumla ya mradi ikiwa ni takriban Shilingi bilioni 25.

Kwa upande wake, Meneja Miradi na Afisa Mipango wa KCMC, Emanuel Biyanchi alisema mradi huo utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda JKCI na nje ya nchi, hivyo kupunguza gharama kubwa kwa wagonjwa na familia zao.

“Karibu asilimia 70 ya wagonjwa wanaopewa rufaa JKCI hushindwa kufika kutokana na changamoto za usafiri na gharama, hivyo huduma zikisogezwa karibu zitakuwa nafuu na rahisi kufikika,” alisema.

Biyanchi aliongeza kuwa taasisi hiyo itakuwa msaada mkubwa katika kupunguza msongamano wa wagonjwa JKCI na kuimarisha huduma za kibingwa nchini.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara, wananchi na wadau wa maendeleo wametakiwa kujitokeza kwa wingi  kushiriki katika harambee itakayofanyika Mei 30 mwaka huu Tanga Beach Resort ili kuchangia kukamilisha mradi huo muhimu wa afya.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com