Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YAPANUA ELIMU YA USALAMA WA CHAKULA KWA WADAU WA CHIPSI NCHINI


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema taasisi hiyo imetoa mafunzo maalumu kwa wadau wanaojihusisha na uandaaji wa viazi vya kukaanga maarufu kama chipsi, kwa lengo la kuhakikisha chakula hicho kinakuwa salama kwa walaji.

Dkt. Katunzi amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za TBS Kanda ya Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo wadau kuhusu kanuni bora za uandaaji wa chipsi na usalama wa chakula.

Amesema chipsi ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa na jamii kutokana na urahisi wa kuandaliwa kwa muda mfupi na kubebwa kirahisi hata kwa watu waliopo katika shughuli za kila siku, hali inayofanya chakula hicho kutumiwa kwa kiwango kikubwa na makundi mbalimbali ya jamii.

“Tumeliita kundi hili mahsusi kwa sababu chipsi ni chakula kinacholiwa na jamii nzima hususan vijana, wanawake na watoto,” amesema Dkt. Katunzi.

Hata hivyo, amesema katika maeneo mengi chipsi huandaliwa katika mazingira yasiyo rasmi na wakati mwingine yasiyo salama kiafya, jambo linaloweza kuhatarisha afya za walaji iwapo hatua stahiki za usalama wa chakula hazitazingatiwa.

Kutokana na hali hiyo, amesema TBS imeona umuhimu wa kutoa elimu kwa wadau hao kuhusu matumizi sahihi ya malighafi wanazotumia, hususan mafuta ya kupikia, namna ya kuyatunza pamoja na kutambua ubora wake ili yaendelee kuwa salama kwa matumizi.

Aidha, amesema mafunzo hayo pia yanagusia matumizi sahihi ya rangi zinazotumika kwenye vyakula pamoja na umuhimu wa kuhakikisha chakula kinachokaangwa kinabaki na ubora wake bila kuhatarisha afya ya mlaji.

Amesema mafunzo hayo yameanza kutolewa jijini Dar es Salaam na yanatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine nchini kwa lengo la kuongeza uelewa kwa wadau wa biashara ya chakula kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama wa chakula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com