Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UHABA WA WATAALAMU WA LUGHA YA ALAMA UNAVYOWANYIMA VIZIWI HAKI YA UZAZI SALAMA



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Katika mapambazuko ya siku mpya, pilikapilika za wodi ya uzazi huanza,
Wahudumu wa afya hukimbizana kuokoa maisha ya mama na mtoto, sauti za maelekezo husikika kila kona huku uchungu wa uzazi ukitangaza mwanzo wa maisha mapya.

Ndani ya wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General), sauti za wahudumu wa afya zinapenya "Sukuma... vuta pumzi... usisukume bado..." ni maelekezo yanayotolewa kwa haraka huku kila sekunde ikihesabika katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Lakini kwa wanawake wenye ulemavu wa kusikia, mazingira hayo hubeba changamoto nyingine kubwa,ukimya wa mawasiliano.

sauti hizo hubaki kuwa midomo inayocheza bila kueleweka. Anachokiona ni wahudumu wakimzunguka, wakionesha ishara ambazo wakati mwingine huzielewa na wakati mwingine hazieleweki,katikati ya uchungu wa uzazi, analazimika kupambana pia na ukimya wa mawasiliano.

Kwao, kujifungua si mapambano dhidi ya uchungu pekee, bali pia ni safari ya kutafuta uelewa wa kila hatua ya matibabu katika mazingira ambayo mara nyingi hayana mtaalamu wa lugha ya Alama.

Ukosefu wa wataalamu hao unaweza kuchelewesha maamuzi muhimu ya kitabibu, kuathiri faragha ya mgonjwa na kuongeza hofu katika kipindi ambacho tayari ni nyeti.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General), wanawake wenye ulemavu wa kusikia wanaeleza kuwa licha ya juhudi za wahudumu wa afya kuwahudumia kwa moyo, changamoto ya mawasiliano bado ipo pale pale.

Hali hii ikanishawishi kumtafuta mkalimani wa lugha ya alama na hatimaye kufanikiwa kufikisha ujumbe wa maumivu ya wajawazito wenye ulemavu huo.

Asia Akilimali ni mkazi wa Dodoma na ni Mwanamke mwenye ulemavu wa kutosikia ,anasema tangu alipozaliwa hajawahi kusikia sauti yoyote,anakumbuka siku yake ya kujifungua kama mojawapo ya siku ngumu zaidi maishani mwake.

"Mimba yangu ya Kwanza nilikuwa kwenye maumivu makali, lakini wakati huohuo nilikuwa nikihangaika kuelewa kila hatua iliyokuwa inafanyika,Wakati mwingine nilihisi taarifa muhimu zinanipita kwa sababu sikuweza kuelewa walichokuwa wakinielekeza," anasema.

Anasema kila mgonjwa ana haki ya kufahamu hatua za matibabu anazopatiwa, lakini haki hiyo huwa ngumu kufikiwa pale mawasiliano yanapokuwa kikwazo.

Kwa Anna Zakayo wa Nzuguni B, anasema ujauzito wake ulihitaji uangalizi wa karibu, lakini mara nyingi alikosa nafasi ya kuuliza maswali kwa sababu hakukuwa na mtu aliyefahamu lugha yake.

"Nilikuwa naambiwa nije na mkalimani,lakini ugonjwa ni siri ya mgonjwa,ningependa hospitalini kuwe na wahudumu wanaojua Lugha ya Alama ili kutusaidia kueleza kwa uhuru bila kumhusisha mtu mwingine," anasema.


Kauli hiyo inaakisi changamoto kubwa inayowakabili wanawake wengi viziwi nchini.

Kukosa wataalamu wa Lugha ya Alama kunawalazimu kwenda hospitalini na ndugu au rafiki kwa ajili ya ukalimani, jambo linaloweza kuvunja haki ya mgonjwa ya faragha na usiri wa taarifa zake za afya.

Tabu Rahidi naye anakumbuka siku ya kujifungua kama safari iliyojaa kusubiri msaada na kutokuelewa kinachoendelea.

"Nilihisi kila hatua ilihitaji nguvu ya ziada,nilisubiri msaada mara nyingi bila kuelewa kinachoendelea,ilikuwa safari ngumu lakini nilifanikiwa kujifungua salama," anasema.

Kwa upande wake, Beatrice John anawapongeza wahudumu wa afya kwa jitihada zao za kuwasiliana kwa ishara na vitendo licha ya ugumu wahudumu wanaokumbana nao, lakini anaamini suluhisho la kudumu ni kuwajengea uwezo wa Lugha ya Alama.

"Ninaamini Serikali ikitoa mafunzo ya Lugha ya Alama kwa wahudumu wa afya na kuwaajiri wataalam katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, huduma zitakuwa bora zaidi kwa watu wenye ulemavu wa kusikia," anasema.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jastus Ng'watalima, anasema Serikali imepiga hatua katika kuboresha miundombinu ya baadhi ya hospitali, lakini bado kuna mapungufu makubwa katika huduma jumuishi.

Anasema changamoto kubwa inayoendelea kuwaumiza watu wenye ulemavu wa kusikia ni ukosefu wa wataalamu wa Lugha ya Alama katika vituo vya kutolea huduma.

"Mgonjwa analazimika kwenda na mkalimani wakati ugonjwa ni siri yake. hii inaweza kuondoa faragha na wakati mwingine kuathiri ubora wa huduma," anasema.

Kwa mujibu wa Katibu huyo wa SHIVYAWATA, Mkoa wa Dodoma una jumla ya watu wenye ulemavu wapatao 299,689, kati yao wanawake ni 152,841 na wanaume 146,847.

Aidha, takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 15 ya watu duniani wanaishi na aina mbalimbali za ulemavu.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Kaimu Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi Maria Lupia anasema hospitali hiyo inaendelea kuboresha huduma kwa wanawake wote bila ubaguzi.

Anasema hospitali imepokea msaada wa vifaa tiba, ikiwemo kitanda maalumu kwa wanawake wenye ulemavu, hatua iliyosaidia kuboresha huduma.

Hata hivyo, anakiri kuwa uhaba wa wataalamu wa Lugha ya Alama bado ni changamoto.

"Mara nyingi tunatumia uzoefu kuwasiliana,tunashukuru wagonjwa wengi wamekuwa wakituelewa na kujifungua salama, lakini tunatambua bado kuna haja ya kuwa na wahudumu wenye ujuzi wa lugha ya alama," anasema.

Mkunga mstaafu, Selina Kusena, anasema changamoto za wajawazito wenye ulemavu haziishii hospitalini pekee.

Anasema wengi wao hukumbana na unyanyapaa na mitazamo hasi kuhusu uwezo wao wa kuwa mama.

Anasisitiza kuwa huduma jumuishi zinapaswa kujumuisha miundombinu rafiki, mawasiliano yanayokidhi mahitaji ya kila mgonjwa pamoja na mafunzo maalumu kwa wahudumu wa afya.

Pamoja na hayo Bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2026/27, Serikali imeeleza kuendelea kuimarisha huduma rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Waziri wa Afya nchini Mohammed Mchengerwa anasema Serikali inaendelea kutekeleza sera ya ujumuishaji katika sekta za afya, elimu, ajira na maendeleo ya kijamii ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma sawa na wananchi wengine.

Katika mjadala wa bajeti hiyo, mmoja wa wadau wa watu wenye ulemavu Hamis Nondwa wa ameiomba Serikali kuongeza huduma za tafsiri ya Lugha ya Alama katika hospitali, shule, mahakama na taasisi nyingine za umma ili kurahisisha mawasiliano kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Anasisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga mfumo rafiki wa utoaji wa huduma za afya kwa makundi yote.

Kwa wajawazito viziwi, uwepo wa wataalamu wa Lugha ya Alama hospitalini si jambo la hiari bali ni hitaji la msingi linaloweza kuokoa maisha.

Mawasiliano sahihi kati ya mgonjwa na mtoa huduma husaidia kufanya maamuzi ya haraka, kulinda usiri wa taarifa za mgonjwa na kuongeza usalama wa mama na mtoto.

Kadiri Tanzania inavyoendelea kuimarisha sekta ya afya, ipo haja ya kuwekeza zaidi katika mafunzo ya Lugha ya Alama kwa wahudumu wa afya na kuajiri wataalamu wa mawasiliano jumuishi katika hospitali na vituo vya afya.

Hapo ndipo haki ya uzazi salama itakapokuwa halisi kwa kila mwanamke, bila kujali hali ya ulemavu.

Maendeleo ya kweli ya sekta ya afya hayapimwi kwa idadi ya majengo au vitanda, bali kwa uwezo wake wa kuhakikisha hakuna mjamzito anayebaki nyuma kwa sababu tu mfumo haukuweza "kusikia" ukimya wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com