Kombaini ya UMITASHUMTA Mkoa wa Pwani kutoka halmashauri tisa za Mkoa huo
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge

NA. ELISANTE KINDULU, KIBAHA

UMOJA wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mkoa wa Pwani umeunda kombaini ya wachezaji wa timu ya mkoa mjini hapa.

Kombaini inaundwa na jumla ya wachezaji 120, walimu 12 na tabibu mmoja.

Michezo iliyoshindaniwa kwaajili ya kuunda kombaini ya mkoa ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa goliboli, na mpira wa wavu.

Michezo mingine ni riadha, miruko, mitupo , kliketi na sanaa za maonesho.

Akizungumza na waanamichezo, walimu na viongozi wa elimu, michezo na utamaduni kutoka halmashauri 9 za mkoa wa pwani, Afisa elimu wa mkoa wa huo, Mwl. Jimmy Nkwamu aliwashukukuru walimu kwa kuinua vipaji vya wanafunzi na kupelekea kupatikana kwa timu ya mkoa.

Aidha Afisa elimu huyo aliwasisitiza viongozi na walimu kuacha kudharau michezo na sanaa na kulazimisha taaluma peke yake kwa mtoto.

"Ukifanya utafiti wanamichezo na wasanii ndio wanaosaidia jamii kwa kujenga nyumba za ibada na shughuli mbalimbali katika jamii kama kina Mbwana Samata, Rose Mhando na wengine wengi. Lakini ni wasomi wangapi wanafanya hivyo! Kuna watu duniani wanatoka kwaajili ya michezo na sanaa. Tusiwazuie watoto kucheza, huwezi kujua Mungu amemuandikia wapi," alisema Afisa elimu huyo.

Jumla ya halmashauri 9 zilishiriki mashindano hayo tangu tarehe 11.5.2025 na kuhitimishwa tarehe 14.5.2025 kwa kuunda kombaini ya mkoa kwa kushirikisha halmashauri za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha manispaa, Kibaha halmashauri, Mafia, Mkuranga, Kisarawe , Kibiti na Rufiji, huku halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ikiibuka mshindi wa jumla.


Afisa elimu wa Mkoa wa Pwani, Mwl. Jimmy Nkwamu akitoa zawadi kwa Wilaya zilizoshinda mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa