Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAFULILA : UZAZI WA MPANGO NI MSINGI WA UCHUMI IMARA


WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Familia Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema changamoto ya uzazi wa mpango ni moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo ya kiuchumi kwa familia nyingi nchini.
Kafulila amesema hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), akieleza kuwa familia nyingi zimekuwa zikizaa watoto wengi kuliko uwezo wa wazazi kumudu gharama za malezi, elimu na afya, jambo linalopunguza uwezo wa watoto hao kuwa rasilimali watu yenye ubora.

Amesema hali hiyo husababisha utegemezi mkubwa kwa Serikali katika utoaji wa huduma za msingi huku familia zikishindwa kufikia ndoto zao za maendeleo.

Aidha, Kafulila amesema kasi ya ongezeko la watu nchini Tanzania ya zaidi ya asilimia 3 kwa mwaka ni kubwa kuliko wastani wa Bara la Afrika ambao ni asilimia 2 pamoja na wastani wa dunia wa asilimia 1.

Kwa mujibu wa Kafulila, Tanzania kwa sasa ipo nafasi ya 81 kwa ukubwa wa uchumi duniani na nafasi ya 165 kwa pato la mtu mmoja mmoja kati ya nchi 193, huku ikiwa nafasi ya 20 kwa idadi ya watu duniani.

Amesema endapo kasi ya ongezeko la watu itaendelea kama ilivyo sasa, ifikapo mwaka 2050 wakati wa kufunga utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, Tanzania itakuwa nafasi ya 14 duniani kwa idadi ya watu.

“Na kama hali itaendelea hivyo, mwaka 2100 Tanzania inaweza kuwa nchi ya tisa duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watu,” amesema Kafulila.

Katika maelezo yake, Kafulila alitolea mfano nchi ya China akisema pamoja na kuwa na uchumi mkubwa duniani, moja ya sababu za mafanikio yake ya kiuchumi ni sera ya kudhibiti uzazi ya mtoto mmoja iliyoanzishwa mwaka 1979/1980.

“Leo China ina ukuaji hasi wa watu (negative growth),” amesema.

Aidha, amesema India licha ya kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani na uchumi mkubwa wa tano duniani, bado kipato cha mtu mmoja mmoja ni kidogo ikilinganishwa na nchi kama Uingereza.

Ameeleza kuwa India ina uchumi wa dola trilioni 4.15 lakini ipo nafasi ya 141 duniani kwa pato la mtu mmoja mmoja, huku Uingereza ikiwa nafasi ya 21 kwa kipato cha mtu kinachozidi dola 57,000 kwa mwaka.

Kafulila amesema Tanzania imejipanga kufikia uchumi wa dola trilioni moja mwaka 2050, lakini kutokana na makadirio ya kuwa na watu milioni 137 wakati huo, pato la mtu mmoja mmoja litakuwa wastani wa dola 7,000 pekee kwa mwaka.

Amesema hata kama Tanzania itafikia uchumi wa dola trilioni moja na kuwa kati ya nchi 35 hadi 45 duniani kwa ukubwa wa uchumi, bado kwa kipato cha mtu mmoja mmoja inaweza kubaki karibu nafasi ya 100 duniani.

Aidha amesema iwapo uchumi utaendelea kukua kwa wastani wa asilimia sita kama ilivyo sasa, mwaka 2050 uchumi wa Tanzania utakuwa takribani dola bilioni 380, huku pato la mtu mmoja mmoja likiwa dola 2,770 kwa mwaka kutokana na ongezeko kubwa la watu.

Kwa mujibu wa Kafulila, hali hiyo inaweza kuifanya Tanzania kubaki miongoni mwa nchi zenye viwango vya chini vya kipato duniani.

Akirejea ripoti ya Hali ya Umasikini na Maendeleo ya mwaka 2014, Kafulila amesema ili Tanzania ifikie malengo ya Dira 2025 katika sekta ya elimu, ilihitajika kuajiri walimu 900,000 kati ya mwaka 2015 hadi 2025, sawa na ajira 90,000 kila mwaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com