Watanzania wamepongezwa kwa kuendelea kushikamana, kuipenda nchi yao na kudumisha amani, utulivu na usalama, suala ambalo limetajwa kama ukomavu wa jamii hasa kipindi cha matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, matukio yaliyotajwa na wananchi kuratibiwa na kuhamasishwa na watu wachache wasioitakia mema nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam leo Jumanne Aprili 14, 2026 akiwemo Bw. Adam Seleman, Mkazi wa Kivule Wilayani Ilala Mkoani Dar Es Salaam, akieleza kwamba uzalendo wa Watanzania pamoja na kumuelewa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa silaha muhimu dhidi ya waliokuwa wakihatarisha amani ya Tanzania.
"Amani ni neno pana sana ila zaidi amani ni uhuru wa kufanya lolote linalokubalika Kikatiba, amani ni upendo, kupendana kwetu kuanzia ndani ya nyumba ndio amani yenyewe,niwaombe watanzania tupendane, tudumishe amani yetu na zaidi niwapongeze Watanzania kwa kumuelewa Rais Samia na kile alichotutahadharisha kuwa wachache wasivuruge amani ya nchi yetu." Amesema Bw. Seleman.
Kwa upande mwingine Bw. Athuman Maziku, Mkazi wa Mvuti Wilayani Ilala ameeleza namna ambavyo amani imemsaidia kuendelea kufanya kazi zake kwa amani na utulivu, akisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki kulinda amani katika maeneo yao, akilaani wale wote wanaopanga na kuratibu njama za kuvuruga amani kwenye jamii.
Amani pia imetajwa katika kujenga mazingira tulivu yanayovutia wawekezaji, utalii, na kuwapa wananchi fursa ya kufanya kazi kwa bidii bila hofu. Inaruhusu rasilimali fedha na nguvu kazi kuelekezwa kwenye miradi ya elimu, afya, na miundombinu badala ya kudhibiti machafuko huku pia Uhuru wa kweli ukitajwa kupatikana kikamilifu pale tu ambapo kuna amani na utulivu.

Social Plugin