Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAPINGA: WATANZANIA WAJITOKEZE SABASABA, BIDHAA ZA NDANI ZAZIDI KUBOREKA



Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amewataka Watanzania kuendelea kutembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema maonesho ya mwaka huu 2026 yameonesha mafanikio makubwa ya maendeleo ya viwanda, ubunifu wa teknolojia na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Akizungumza Julai 08, 2026 baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho hayo, Kapinga amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa kiasi kwamba Serikali inatafakari kuongeza siku moja ya maonesho ili kutoa nafasi kwa wananchi wengi zaidi kushiriki na wafanyabiashara kuendelea kufanya biashara.

Amesema ukubwa wa maonesho hayo unamlazimu kuyatembelea mara kwa mara kwa kuwa haiwezekani kuona mabanda yote kwa siku moja, huku akieleza kuridhishwa na namna waoneshaji walivyojiandaa na ubora wa bidhaa zinazooneshwa.

Waziri Kapinga amesema maonesho ya mwaka 2026 yamebeba teknolojia mbalimbali za kisasa, ikiwemo magari yanayotumia umeme, magari ya mseto (hybrid), magari yanayotumia gesi asilia (CNG) kwa asilimia 100 pamoja na mitambo ya kisasa inayotumia umeme, hatua inayoonesha ukuaji wa sekta ya viwanda na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Aidha, amesema bidhaa za ndani zimeendelea kuongezeka ubora, hususan katika thamani na vifungashio, jambo linalodhihirisha mafanikio ya uwekezaji wa Serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza uzalishaji wa ndani.

"Wananchi waendelee kujitokeza kutembelea Sabasaba. Fursa zilizopo mwaka huu ni nyingi zaidi, hivyo ni wakati mzuri wa kujifunza, kufanya biashara na kuona maendeleo ya viwanda vya Tanzania," amesema Kapinga.

Ameongeza kuwa iwapo uamuzi wa kuongeza siku moja ya maonesho utapitishwa, utalenga kuwapa wananchi, hasa wanaokuwa kazini siku za kawaida, nafasi zaidi ya kutembelea maonesho hayo na kunufaika na fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com