Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKONDA AWATAKA WANAHABARI KUJIRIDHISHA NA TAARIFA

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuhakikisha wanajiridhisha na vyanzo vyao vya taarifa kabla ya kuzisambaza kwa umma ili kuepuka migogoro na upotoshaji unaoweza kujitokeza. 

Akizungumza jijini Arusha leo Aprili 30, 2026, katika kilele cha siku ya tatu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Waziri Makonda amesisitiza umuhimu wa weledi huo akibainisha kuwa mchango wa vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kusaidia maendeleo ya nchi na kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Aidha, Waziri Makonda amewataka wadau wa sekta ya habari kubadili mkakati na kuachana na ajenda za kutangaza au kusifia watu binafsi, badala yake wajikite katika kutangaza fursa nyingi za kiuchumi zilizopo nchini kwa maslahi ya Taifa. 

Amekemea kasumba ya baadhi ya wanahabari kuwaandika vyema watu wasio na sifa njema au wala rushwa, akitolea mfano kuwa kuna uhaba wa waandishi wanaoangazia sekta muhimu kama utalii na kilimo ikilinganishwa na wale wanaopoteza muda mwingi kwenye masuala ya siasa pekee.

Katika kuelekea maboresho ya sekta hiyo, Mhe. Makonda amethibitisha kuwa Serikali imepokea mapendekezo yote 15 yaliyowasilishwa na wadau na imeahidi kuyafanyia kazi kwa ushirikiano wa karibu. 

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Gerson Msigwa, amebainisha kuwa maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kutathmini uhuru wa habari na kukutana na washirika wa maendeleo ili kujadili mabadiliko ya utendaji na namna ya kuwaendeleza watayarishaji wa maudhui katika mazingira ya sasa ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Mkurugenzi wa Tech and Media Convergency (TMC), Bi. Asha Abinallah, amewasilisha vipaumbele vya wadau vikihimiza Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Mfuko wa Habari na kuweka sera rafiki za uwekezaji. 

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuendelea kutimiza wajibu wake, hususan katika kuwajengea wanahabari uwezo wa kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI) ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya ulimwengu wa habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com